Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, kitendo hicho kimeibua mjadala mkubwa kuhusu haki za kidini katika nchi hiyo ya Ulaya inayodai kuwa kitovu cha uhuru.
‘Ni vipi unaweza kutathmini uwezo wa mtu kufanya kazi kwa mujibu wa uzingatiaji mafundisho ya kidini?’ amehoji Mohand Yanat, wakili wa Waislamu hao waliofutwa kazi.
Walimu hao wanne Waislamu walikuwa wakitoa mafunzo katika kambi ya watoto ya Geenevilliers nje kidogo ya mji mkuu wa Ufaransa, Paris.
Maafisa kielimu katika eneo hilo wamedai kuwa kutokula na kunywa kunawazuia waalimu kutekeleza majukumu yao.
Waislamu nchini Ufaransa wamelalamikia vikali kitendo hicho na kusema ni ukiukwaji wa wazi wa haki za kuabudu.
Baraza Kuu la Waislamu Ufaransa (CFCM) limekosoa vikali hatua ya kuwafuta kazi Waislamu hao na kusema saumu ni haki ya kimsingi ya Waslamu. Msemaji wa CFCM Abdallah Zekri amesisitiza kuwa uhuru wa kuabudu ni haki ya kimsingi na kwa vyovyote vile hakuna haki ya kumpiga mtu marufuku kutekeleza maamrisho ya dini yake.
Waislamu Ufaransa wamekuwa wakilalamika kuwa wanabaguliwa sana. Mwaka 2004 Ufaransa ilipiga marufuku uvaaji wa Hijabu katika maeneo ya umma na nchi kadhaa za Ulaya pia ziliiga mfano huo mbaya.
Waislamu Ufaransa pia wanawekewa vizingiti katika ujenzi wa misikiti.
1068030