Kwa mujibu wa idara ya mawasiliano ya umma ya kituo hicho, mashindano hayo yatafanyika katika makundi mawili ya hifdhi na kiraa tarehe 12 na 13 za mwezi huu.
Lengo la kufanyika mashindano hayo ambayo huandaliwa kila mwaka katika kituo hicho limetajwa kuwa ni kufahamu maana ya ujumbe wa Qur'ani Tukufu na kufarijika na kitabu hicho cha wahyi, kueneza utamaduni mtukufu wa Qur'ani katika jamii ya Kiislamu, kuleta umoja katika jamii ya Kiislamu, kuboresha viwango vya usomaji na hifdhi ya Qur'ani Tukufu na kuleta mvuto kati ya wasomi na mahafidh wa kitabu hicho cha mbinguni.
Washiriki wa kundi la hifdhi watagawanywa katika makundi kadhaa ya hifdhi ya Qur'ani nzima, juzuu 10, juzuu 5, juzuu 4, juzuu 3, juzuu 2 juzuu 1 na hatimaye hifdhi ya sura ya ar-Rahman.
Kundi la kiraa litawashirikisha washindani wanaume walio na umri wa miaka 14 kwenda juu, na jingine ambalo litagawanyika katika makundi mengine mawili ya mabinti na wavulana walio na umri wa miaka 10 hadi 14 na wengine walio na umri wa miaka 15 kwenda juu.
Washindi wa mashindano hayo wataarifishwa na kutunukiwa zawadi tarehe 14 Agosti. 1070217