IQNA

Tamasha la nne la kaligrafia ya Qur'ani kufanyika Imarati

17:09 - August 11, 2012
Habari ID: 2390313
Duru ya nne ya tamashala la kimataifa la kaligrafia ya Qur'ani Tukufu imeapangwa kufanyika siku ya Jumatatu tarehe 13 Agosti katika hoteli ya Grand Hyatt mjini Dubai kwa udhamini wa Wizara ya Utamaduni, Vijana na Ustawi ya Imarati.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la nchi hiyo WAM, tamasha hilo linalotazamiwa kumalizika siku ya Jumatano litawashirikisha wanakaligrafia 30 kutoka nchi 12 za dunia. Kila mmoja wa wanakaligrafia hao ataandika kwa mkono juzuu moja ya Qur'ani kwa kutumia hati maalumu za kaligrafia ambapo wino, aina na ukubwa wa hati itakayotumika katika uandishi huo vitakuwa vya aina moja kati ya waandishi wote.
Hakam al-Hashimi, Naibu Waziri wa Utamaduni, Vijana na Ustawi wa Imarati amesema kuhusu jambo hilo kwamba kamati ya waamuzi wa tamasha hilo itawajumuisha wanakaligrafia mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu ikiwa ni pamoja na Bahiya Dawoud al-Farjawi kutoka Iraq na Ubeida Muhammad Swalih al-Banki kutoka Syria.
Al-Hashimi amesema tamasha hilo litakalofanyika katika mwezi huu mtukufu wa Ramdhani pia litajumuisha vikao tofauti ambavyo vitajadili hati tofauti za uandishi wa Qur'ani kwa mkono na umaridadi wa hati hizo.
Wanakaligrafia kutoka Iraq, Misri, Syria, Iran, Saudi Arabia, Jordan, Palestina, Algeria, Uturuki, Uingereza na Ujerumani wanatazamiwa kushiriki katika tamasha hilo. 1075475
captcha