IQNA

Mtume Muhammad (SAW) Alikuwa ‘Kiumbe Mkamilifu Zaidi Aliyepambwa Kwa Sifa za Juu za Kibinadamu’

18:21 - September 11, 2025
Habari ID: 3481213
IQNA – Mwanazuoni mwandamizi wa Waislamu wa madhehebu Kishia nchini Iraq, Ayatullah Mkuu Mohammad al-Yaqoobi, ameadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) kwa kutoa wito wa kumfuata Mtume katika maisha na jamii.

Katika tamko alilolitoa kwa Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), Ayatullah, al-Yaqoobi alisisitiza kuwa kumbukumbu ya mwaka huu ina umuhimu wa kipekee, kwani inasadifiana na kutimia kwa karne 15 tangu “rehema hii ya Allah kutunukiwa ulimwengu.” 

Akinukuu Qur’an Tukufu, alieleza kuwa Mtume Muhammad (SAW) aliwasilishwa kama mfano bora wa kuigwa na wanadamu.

“Mwenyezi Mungu Mtukufu alimchagua Mjumbe Wake mtukufu kuwa kielelezo chema kwetu kwa sababu ndiye kiumbe mkamilifu zaidi aliyepambwa kwa sifa za juu za kibinadamu, na kila sifa ya ukamilifu ilikusanyika ndani yake,” alisema Ayatullah al-Yaqoobi.

Akinukuu aya ya 21 ya Surah al-Ahzab — “Hakika katika Mtume wa Mwenyezi Mungu kuna kielelezo chema (ruwaza njema) kwa anayemtarajia Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana” — marja’ alisisitiza kuwa aya hiyo haikuhusu tu waumini wa wakati wa Mtume, bali ni wito kwa wanadamu wote. “Kila mmoja anaitwa kufuata haki na kuifikia hakika,” alifafanua.

Aidha, alibainisha kuwa mwenendo wa Mtume Muhammad (SAW) ulikuwa umejikita sana katika Qur’an kiasi kwamba mke wake alimtaja kuwa ni mfano hai wa mafundisho yake. “Tabia yake ilichukuliwa kutoka katika Qur’an,” alisema al-Yaqoobi, akiongeza kuwa hilo lilimfanya kuwa mwangaza wa uongofu wa kimungu.

Kiongozi huyo wa kidini alieleza kuwa kumchukua Mtume (SAW) kama mfano si suala la ibada ya mtu binafsi tu, bali ni jukumu la pamoja linalolinda umma wa Kiislamu.

Alionya kuwa kupuuza kanuni hii kumeacha Waislamu wengi wakiwa dhaifu, wakigawanyika, na wakitegemea wengine, huku wakivutwa na “mifano mibaya” kama vile makundi yenye misimamo mikali yanayopotosha Uislamu na kuwafanya watu wakimbie mafundisho yake ya kweli.

Akinukuu maneno ya Imam Ali (AS), al-Yaqoobi alitoa tahadhari dhidi ya kuwafuata viongozi waliopotea: “Msiruhusu upotofu wa wengine uwapotoshe kutoka njia ya haki.” Aliongeza kuwa historia imethibitisha jinsi uongozi wa kifisadi unavyoweza kupoteza mataifa yote.

Marja’ huyo pia alihusisha umuhimu wa kumwiga Mtume (SAW) na maandalizi ya kurejea kwa Imam al-Mahdi. “Moja ya majukumu yetu ni kuandaa njia ya kudhihiri kwa baraka hiyo kwa kuishawishi jamii kuhusu Uislamu wa kweli wa Muhammadi,” alisema. Njia bora ya kufanikisha hilo, alisisitiza, ni kuishi kwa mfano wa Mtume katika maisha ya kila siku.

Ayatullah Al-Yaqoobi alihitimisha ujumbe wake kwa dua ya ushindi wa Uislamu na uthabiti katika njia ya Mwenyezi Mungu: “Tunamuomba Mwenyezi Mungu  ya zote, na atufanye tuwe thabiti katika njia yake iliyonyooka.”

3494552

captcha