IQNA

Umoja wa Mataifa walaani mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia Pakistan

0:12 - August 27, 2012
Habari ID: 2399453
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa taarifa akilaani mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika shambulizi lililofanywa dhidi ya basi walimokuwa wakisafiria nchini Pakistan.
Katika taarifa hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kusikitishwa na kuchukizwa na mashambulizi kama hayo yanayofanyika kwa makusudi dhidi ya watu wa Pakistan kwa sababu tu ya itikadi zao na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga, serikali na watu wa Pakistan.
Watu waliokuwa na silaha Alkhamisi iliyopita walishambulia basi moja lililokuwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia na kuwapiga risasi watu waliokuwamo. Watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulizi hilo.
Wasafiri hao walikuwa njia kutoka mji wa Rawalpindi wakielekea katika mji wa Galgat wenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Katika upande mwingine Waislamu wengine wasiopungua watatu wa Kishia wameuawa katika hujuma iliyofanywa na watu waliokuwa na silaha katika mji wa Quetta katika jimbo la Baluchistan huko kusini magharibi mwa Pakistan.
Mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia pia wameuawa katika mashambulizi mbalimbali yaliyofanywa na makundi ya Kiwahabi kwenye maeneo tofauti ya Pakistan.
Wakati huo huo maandamano ya kupinga mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Pakistan yameendelea kufanyika katika nchi mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na huko Marekani, Uingereza na Canada. 1084156
captcha