Baada ya kutengenezwa na kuoneshwa filamu ya "Innocence of Muslims" huko Marekani, Sheikh wa al Azhar amemwandikia barua ya wazi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akisisitiza juu ya udharura wa kubuniwa sheria za kimataifa za kupiga marufuku kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu.
Sehemu moja ya barua hiyo imesema kuwa, sheria hizo zinapaswa kuainisha adhabu kwa watu wanaovunjia heshima na kuwakebehi Waislamu na matukufu ya kidini, kwani vitendo kama hivyo vinahatarisha amani na usalama wa kimataifa.
Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unawajibika kulinda amani na usalama wa dunia na kukabiliana na aina zote za ukatili na utumiaji mabavu.
Amesema iwapo sheria hizo zitapasishwa hakutashuhudiwa tena matukio ya hatari kama haya ya sasa.
Sheikh Ahmad Tayyib amelaani tena filamu ya Kimarekani inayovunjia heshima matukufu ya Kiislamu na kuwataka Waislamu kuwa watulivu na kutohatarisha maisha ya watu wasiokuwa na hatia. 1099184