Barani Asia mamilioni ya wananchi wa Pakistan walifanya maandamano jana katika miji tofauti ya nchi hiyo wakilaani filamu na vibonzo hivyo. Waislamu hao waliandamana katika miji kama Lahore, Islamabad, Karachi, Rawalpindi na Pishawar wakitaka kuvamia balozi za Marekani na Ufaransa ambako walikabiliana na polisi na askari usalama.
Waandamanaji hao waliokuwa na hasira walilaani vitendo vya kuvunjiwa heshima Mtume wa Mwenyezi Mungu katika nchi za Magharibi hususan filamu ya Kimarekani na kutaka watayarishaji na wasambazaji wake wapewe adhabu kali. Vilevile wameitaka serikali ya nchi hiyo ichukue hatua kali dhidi ya njama hiyo mpya ya Marekani na Wazayuni kama kumfukuza balozi wa Washington nchini humo na kufunga ubalozi wa Marekani.
Maandamano ya wananchi wa Pakistan yalikuwa makubwa sana na kusababisha ghasia na mapigano kati ya waandamanaji hao na askari usalama na inaripotiwa kuwa watu 23 wameuawa na wengine 200 kujeruhiwa.
Mjini Kabul, Afghanistan mamilioni ya Waislamu waliandamana jana Ijumaa wakilaani kuvunjiwa heshima Mtume wa Uislamu. Waandamanaji hao walisema kuwa filamu na vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW) ni utumiaji mbaya wa uhuru wa kusema na kujieleza na vinahatarisha amani na usalama wa kimataifa.
Maelfu ya Waislamu pia walifanya maandamano jana nchini Afrika Kusini wakipinga vitendo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu katika nchi za Magharibi. Waislamu wa mji wa Pretoria waliokuwa wakipiga nara dhidi ya Marekani na utawala haramu wa Israel, wametoa wito wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya watayarishaji na wasambazaji wa filamu inayomvunjia heshima Mtume wa Mwenyezi Mungu. Maandamano kama hayo ya mamilioni ya watu yamefanyika pia katika nchi za Indonesia, Malaysia na Bangladesh.
Huko Tanzania maelfu ya waumini wa dini ya Kiislamu waliandamana jana na kukusanyika kwenye viwanja vya Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam ambako walitoa tamko dhidi ya wanaoshambulia na kunyanyasa Uislamu.
Maandamano hayo yamefanyika kupinga filamu iliyotengenezwa Marekani ikimkashifu Mtume Muhammad (SAW).
Akitoa tamko la Waislamu, Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Shekhe Ponda Issa Ponda ameitaka serikali ya Tanzania kuzuia mitandao ya intaneti, dvd na mianya mingine ya kuonyesha filamu hiyo ya kumkashifu Mtume, sambamba na kutaka ubalozi wa nchi hiyo ufungwe.
Sheikh Ponda amesema, kuanzia sasa Waislamu watasusia bidhaa zote zinazotengenezwa na Marekani pamoja na Israel na balozi zao nchini Tanzania zinapaswa kufungwa, la sivyo Waislamu watachukua hatua zaidi. 1103701