Viongozi hao pia wametoa changamoto kwa Rais Barack Obama wa Marekani baada ya kutetea kitendo cha kuonyeshwa filamu inayomtusi Mtume Muhamamd (saw) kwa kutumia kisingizio cha uhuru wa kusema na kujieleza.
Hatua hiyo ya viongozi wa nchi za Kiislamu wanaoshiriki katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York imechukuliwa baada ya Rais wa Marekani kulaani alichokiita “ukatili na misimamo mikali ya kidini” iliyotokea kote duniani baada ya kutengenezwa na kuonyeshwa filamu ya Kimarekani inayomvunjia heshima Mtume wa Uislamu.
Obama pia amedai kuwa kuzuiwa kuonyeshwa filamu hiyo inayovunjia heshima matukufu ya kidini au kukabiliana na uenezaji wake kunakiuka katiba ya nchi yake ambayo amesema, inalinda uhuru wa kusema na kujieleza.
Rais wa Indonesia Susilo Bambang Yudhoyono ambaye amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ametoa changamoto kwa matamshi hayo ya Obama akisisitiza kuwa, filamu hiyo ni mfano mwingine wa vitendo vinavyotusi na kuvunjia heshima matukufu ya kidini.
Rais wa Indonesia amesema kuwa, kwa mujibu wa Tangazo la Haki za Binadamu, uhuru wa kusema na kujieleza si mutlaki bali una mipaka, na watu wote wanapaswa kuheshimu masuala ya kimaadili na nidhamu ya umma.
Susilo Bambang ametoa wito wa kubuniwa sheria za kimataifa za kuzuia vitendo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini.
Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari pia ameutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kukomesha uchochezi unaofanywa dhidi ya Waislamu.
Zardari amesema, jamii ya kimataifa haipaswi kunyamaza kimya bali inalazimika kukabiliana na vitendo hivyo vinavyotishia amani ya kimataifa kwa kutumia vibaya uhuru wa kusema na kujieleza.
Rais wa Afghanistan Hamid Karzai ambaye pia amehutubia kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amelaani vikali filamu ya Kimarekani inayomvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) na kusema, propaganda chafu zinazolenga Uislamu zinatia wasiwasi na kutishia amani ya kimataifa.
Filamu ya Kimarekani inayomvunjia heshim Mtume Muhammad (saw) imezusha wimbi kubwa la hasira na maandamano kote duniani. Waislamu wanaitaka serikali ya Marekani iwaombe radhi na kuwafikisha mahakamani walioitengeneza na kuisambaza. 1107817