Mkutano huo umefunguliwa Jumamosi Desemba 15 na makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal ambaye aliwataka Maulamaa wa Kiislamu wajadili njia za kuweka mustakabali mzuri wa Waislamu. Aidha amewataka Maulamaa wa Kiislamu kujadili kuhusu njia za kuhakikisha kuwa Waislamu na Wakristo wanaishi kwa kuheshimiana.
Makamu wa Rais wa Tanzania alisisitiza umuhimu wa elimu kwa Waislamu na kusema itawawezesha kutatua matatizo yanayowakabili.
Alitoa changamoto kwa wanazuoni wa Kiislamu kuangalia ni vipi utandawazi hautoathiri imani na maadili ya waumini, lakini pia ni jinsi gani waumini watanufaika na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, yaliyofikiwa na mwanadamu hivi sasa.
Akizungumza katika mkutnao huo Rais wa Jumuiya ya Wanazuoni Tanzania, Sheikh Suleiman Kilemile amesema mkutano huo wa siku tatu, umekusudia kuzungumzia masuala mbalimbali yatakayojenga misingi ya dini hiyo ndani na nje ya Bara la Afrika.
Alisema mkutano huo unahudhuriwa na maulamaa na mubalighina wa Kiislamu kutoka nchi takribani 24 zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara na nje ya Bara la Afrika.
1154941