IQNA

11:46 - January 26, 2013
Habari ID: 2486170
Sayyid Hassan Nasrullah:

Kuvunjiwa heshima Mtume SAW ni changamoto kwa Umma wa Kiislamu

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah nchini Lebanon amesema kuwa, imepangwa mikakati maalumu ya kumvunjia heshima Mtume Mtukufu Muhammad SAW na dini tukufu ya Kiislamu na jambo hilo linatoa changamoto kubwa kwa umma wa Kiislamu.

Akihutubia kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Umoja wa Kiislamu na kuzaliwa Mtume Mtukufu SAW huko kusini mwa Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah amesisitiza kuwa Qur'ani Tukufu inatulingania kufanya mazungumzo baina yetu, lakini suala la kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu kamwe halikubaliki kwa mtu yeyote yule.
Sayyid Nasrullah ameongeza kuwa changamoto nyingine inayoukabili ulimwengu wa Kiislamu ni ongezeko la mapigano na machafuko kwenye nchi za ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu. Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kuwa, machafuko na mapigano mengi yanajiri kwa malengo ya kisiasa, ingawa yanafanyika kwa kisingizio cha umadhehebu na udini. Ameongeza kuwa,mapigano hayo yanafanyika kwa lengo la kujipatia madaraka na wala hayana mahusiano yoyote na Uislamu, Ukristo na wala Usuni na Ushia.
Sayyid Nasrullah ameongeza kuwa, mapigano yanayotokea katika nchi mbalimbali kama vile Syria, Iraq, Yemen, Tunisia, Libya Lebanon na Misri hayana maslahi kwa mataifa hayo bali yanaongeza maafa kwa nchi na wananchi na kuzinufaisha nchi za Magharibi na hasa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
1177415
captcha