IQNA

20:52 - March 09, 2013
Habari ID: 2508655
Hamas:

Safari ya Obama Baitul Muqaddas ni tangazo la vita

Mushir al Masri ambaye ni miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa safari iliyopangwa kufanywa na Rais Barack Obama wa Marekani huko Baitul Muqaddas, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kwenda katika Msikiti wa Al Aqsa ni sawa na tangazo la vita dhidi ya Wapalestina na kuchochea hisia za Waislamu kote duniani.

Mushir al Masri ambaye ameshiriki katika maandamano ya kulaani kitendo cha askari wa Israel cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu ndani ya Msikiti wa Al Aqsa amesema safari iliyopangwa kufanywa na Obama katika mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na Israel ni tangazo la vita dhidi ya Wapalestina na uchochezi wa hisia za Umma wa Kiislamu. Al Masri amemtaka Rais wa Marekani atupilie mbali nia yake ya kutembelea Msikiti wa Al Aqsa na kusema msikiti huo ni haki ya taifa la Palestina.
Mushir Al Masri pia ameutaka Umma wa Kiislamu na Kiarabu kuulinda na kuutetea msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.
Ripoti zinasema kuwa idadi kubwa ya askari wa utawala ghasibu wa Israel jana walivamia eneo la msikiti huo baada tu ya Waislamu kukamilisha Sala ya Ijumaa na kuwafyatulia risasi za plastiki. 1201339
captcha