Muhammadu Buhari amebainisha kwamba, madai ya Boko Haram ya kuzihusisha harakati zake na dini hayana ukweli wowote kwani hakuna itikadi ya dini yoyote ile ambayo inayohalalisha jinai au kuua watoto wa shule. Rais huyo mteule wa Nigeria alimshinda Goodluck Jonathan katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni. Buhari amesisitiza kuwa, Boko Haram ni kundi la kigaidi na kwamba, serikali yake itapambana na kundi hilo kwa mujibu wa mbinu na mikakati ya kukabiliana na magaidi. Muhammadu Buhari amemtuhumu Rais Gooluck Jonathan anayeondoka kwamba, ameshindwa kukabiliana vilivyo na tishio la usalama linaloikabili nchi hiyo. Buhari amesisitiza kuwa, wakati umefika wa kufanyika mabadiliko na mageuzi makubwa nchini humo.../EM