IQNA

Machafuko katika Msikiti wa Al Aqsa

18:47 - August 02, 2015
Habari ID: 3338073
Machafuko yameibuka leo Jumapili katika Msikiti wa Al Aqsa, eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu, mjini Quds (Jerusalem) siku mbili tu baada ya mtoto mchanga Mpalestina kuchomwa moto na kuuawa na walowezi wa Kiyahudi.

Vijana wa Kipalestina wamewarushia mawe wanajeshi wa Israel huku waandamanaji wakiwa wamebeba picha za mtoto mchanga wa miezi 18 aliyeuawa na masetla Waisraeli katika hujuma ya jinai huko katika Ukingo wa Magharibi.
Kumeripotiwa wimbi kubwa la maandamano katika ardhi za Palestina tokea jinai hiyo ya Ijumaa.
Mapema Ijumaa walowezi wa Kiyahudi walishambulia kijiji cha Duma katika Ukingo wa Magharibi huko Palestina na kuchoma moto nyumba mbili za Wapalestina. Katika shambulizi hiyo la kinyama Wazayuni hao wamemchoma moto na kumuua mtoto mdogo aliyekuwa na umri wa miezi 18 kwa jina Ali Saad Dawabsha na kuwajeruhi vibaya wazazi na ndugu yake mwenye umri wa miaka minne. Jinai hiyo ya kutisha imekabiliwa na upinzani mkali wa Wapalestina na fikra za waliowengi duniani.
Makundi mbalimbali ya mapambano ya ukombozi wa Palestina yamelaani jinai hiyo na kuapa kwamba yatalipiza kisasi. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kwamba itajibu vikali kitendo hicho cha Wazayuni cha kumchoma moto hadi kufa mtoto mdogo wa Palestina.../mh

3336961

captcha