Tukio hilo liliibuka wakati kijana Ahmed Mohammed mwenye umri wa miaka 14 katika mji wa Irving jimbo la Texas, alipotiwa mbaroni na polisi ya mji huo kutokana na kutengeneza saa na kumwonyesha mwalimu wake shuleni. Mmoja wa walimu wa shule hiyo ambaye aliifananisha na bomu saa hiyo iliyotengenezwa na kijana huyo hodari, alitoa taarifa kwa polisi wa mji wa Irving, suala ambalo lilipelekea kutiwa kwake mbaroni kijana Ahmed na kutiwa pingu. Kilichomsaidia kijana huyo mwenye asili ya Sudan, ni fikra za waliowengi katika mji huo zilipata habari ya mwenendo huo wa kibaguzi haraka kupitia mitandao ya kijamii na kwa utaratibu huo akaachiliwa huru saa moja baada ya kutiwa mbaroni.
Pamoja na hayo, tukio hilo la utengenezaji saa wa kijana huyo Mwislamu mwenye asili ya Kiafrika, limedhihirisha ni kwa kiasi gani hujuma dhidi ya Waislamu na vitendo vya udhalilishaji dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika wanavyodhalilishwa katika jamii ya Marekani. Baada ya tukio la Septemba 11 mwaka 2001, wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na kuidhihirisha dini hiyo kuwa ni tishio, lilishika kasi zaidi nchini humo ambapo licha ya kupita miaka 14 sasa tangu kujiri kwake, limeyafanya machungu maisha ya mamilioni ya Waislamu wanaoishi nchini Marekani. Katika kipindi hicho, kumeripotiwa matukio mbalimbali ya kubaguliwa na kunyanyaswa Waislamu katika nchi hiyo inayojinadi kuwa mtetezi wa haki za binaadamu duniani. Kiasi kwamba, hata baadhi ya watu wamezuiliwa kusafiri katika ndege za Marekani, kutokana na kukutwa na maandishi ya Kiarabu au kuzungumza lugha hiyo ambayo ni moja ya lugha za nchi za eneo la Mashariki ya Kati. Siku chache baada ya tukio la Septemba 11, Mmarekani mmoja Singasinga mwenye asili ya India aliuawa na Wamarekani wenye misimamo mikali kutokana na kuvaa vazi la kilemba kichwani mwake. Vilevile dereva mmoja aliuawa kwa kuchomwa kisu na askari aliyekuwa amerejea Marekani kutoka Afghanistan kwa sababu tu ya kuwa Mwislamu.
Chuki dhidi ya dini ya Uislamu ilizidi kushika kasi kiasi kwamba, hata kutembelea maktaba za kijamii na kuchukua kitabu chenye maudhui za dini hiyo ya mbinguni huko Marekani kwa Waarabu na Waislamu kunawaweka watu hao katika orodha ya washukiwa wa ugaidi au washirika wa magaidi. Katika anga hiyo haitakuwa ajabu kwa kijana Mwislamu mwenye asili ya Afrika, kudhaniwa vibaya kama kuwa ametengeneza bomu na kadhalika. Baada ya kuenea sana ukosoaji na upinzani wa walio wengi kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii dhidi ya hatua ya polisi ya Marekani dhidi ya kijana huyo, Rais Barack Obama wa Marekani, alieleza kusikitishwa na tukio hilo na kuamua kumwalika kijana Ahmed Mohammed ikulu ya White House.
Pamoja na hayo ni jambo lililo mbali kwamba hatua hiyo ya Obama ya kumwalika kijana huyo White House, itaandaa mazingira ya kupunguza wimbi la chuki na hujuma dhidi ya dini ya Uislamu na ubaguzi dhidi ya Waislamu na raia wenye asili ya Kiafrika nchini Marekani. Ikumbukwe kuwa kwa miaka kadhaa sasa, asasi rasmi na zisizo rasmi nchini Marekani zimekuwa zikiufananisha Uislamu ugaidi, kufurutu mipaka na ukatili. Miaka 14 iliyopita, George W. Bush rais wa wakati huo nchini Marekani alilitaja tukio la Septemba 11 kuwa ni Vita vya Msalaba katika zama hizi, ambavyo vinakumbushia vita vilivyojiri baina ya Waislamu na Wakristo katika karne za kati. Katika miaka yote ya baada ya tukio hilo la Septemba 11, kila kulipotokea mlipuko au shambulizi lolote ambalo ndani yake yumo Mwislamu au Mwarabu, basi haraka sana vyombo vya Magharibi hulitaja tukio hilo kuwa shambulizi la kigaidi. Hii ni katika hali ambayo kunapotokea tukio kama hilo hilo lakini likawa limefanywa na asiyekuwa Mwislamu vyombo hivyo hulitaja tukio hilo kuwa ni hujuma ya kawaida tu.../mh