IQNA

Mwana wa Qari Maarufu Sheikh Abdul Basit Abdul Samad Afariki Dunia Huko Cairo

19:23 - November 01, 2025
Habari ID: 3481447
IQNA – Mwana wa qari mashuhuri wa Qur’ani kutoka Misri, Sheikh Abdul Basit Abdul Samad (rahimahullah), ambaye sauti yake imehifadhiwa katika nyoyo za Waislamu duniani kote, amefariki dunia mjini Cairo siku ya Ijumaa, tarehe 31 Oktoba 2025.

Kifo cha Essam Abdul Basit Abdul Samad kilitangazwa rasmi na ndugu yake, Sheikh Yasser Abdul Basit Abdul Samad, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maqari wa Cairo.

Katika taarifa rasmi, Sheikh Yasser alisema: “Kwa nyoyo zilizojaa imani kwa qadar ya Mwenyezi Mungu, tunamwomboleza kipenzi chetu Essam Abdul Basit Abdul Samad, aliyefariki alfajiri ya leo. Mwenyezi Mungu amsamehe, amrehemu, na amuingize Peponi.”

Swala ya jeneza iliswaliwa baada ya swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Mostafa Mahmoud uliopo Mohandessin, ikifuatiwa na maziko yaliyohudhuriwa na wanafamilia na wapenzi wa familia ya qari huyo mashuhuri.

Waziri wa Wakfu wa Misri, Dkt. Osama Al-Azhari, alituma salamu za rambirambi kwa familia hiyo, akiomba rehema za Mwenyezi Mungu kwa marehemu na subira kwa jamaa zake.

Jumuiya ya Maqari wa Qur’ani nchini Misri pia ilitoa taarifa ya maombolezo, ikiwapa pole wanafamilia wakiwemo Sheikh Tariq Abdul Basit Abdul Samad na Sheikh Yasser Abdul Basit Abdul Samad.

Watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii walieleza huzuni zao na kutoa heshima kwa marehemu.

Sheikh Abdul Basit Abdul Samad (rahimahullah) ataendelea kuwa nembo ya usomaji wa Qur’ani katika ulimwengu wa Kiislamu, akijulikana kwa umahiri wake wa kipekee na athari ya kiroho inayodumu vizazi hadi vizazi.

3495219

Habari zinazohusiana
captcha