Rais Rouhani ameyasema hayo leo mjini Tehran alipowasili baada ya kukatiza safari yake katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York. Rais Rouhani amesema Saudi Arabia inapaswa kutekeleza majukumu yake kimataifa sambamba na kubainisha sababu za kutokea maafa hayo.
Rais wa Iran ameongeza kuwa, maafa ya Mina si ya kawaida na kwamba Saudi Arabia inapaswa kusambaza picha zilizonaswa na kamera wakati wa tukio hilo. Rais Rouhani amekosoa pia namna vyombo vya habari vinavyoakisi habari za maafa ya Mina na kuongeza kuwa, baadhi ya vyombo vya habari vya Saudia Arabia vinarusha hewani kanda za video ambazo zinawavunjia heshima Waislamu.
Kwingineko Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka Saudi Arabia kukubali majukumu yake kuhusiana na maafa ya kuhuzunisha ya vifo vya mamia ya mahujaji wa Irani na Waislamu wa maeneo mengine duniani waliokwenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Makka.
Dakta Hassan Rouhani ameyasema hayo katika hotuba yake kwenye Mkutano wa 70 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani. Ameashiria maafa ya kufariki dunia mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Mina nchini Saudi Arabia na kusema: Inasikitisha kwamba mwaka huu maelfu ya mahujaji wa Iran na wasio Wairani wamekuwa wahanga wa uzembe na usimamizi mbaya wa mafisa wa Hija nchini Saudi Arabia. Amesisitiza kuwa Iran itafuatilia haki za mahujaji wa Iran waliopatwa na maafa nchini Saudia na amewataka viongozi wa serikali ya Riyadh kutekeleza majukumu yao ya kuwadhaminia maafisa wa ubalozi wa Iran uwezo wa kuwapata haraka mahujaji waliotoweka na kurejesha nchini maiti za waliofariki dunia.
Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imetangaza kuwa, idadi ya Mahujaji walipoteza maisha katika maafa ya Mina imefikia 4,173..../mh