IQNA

Hamas na Harakati ya Jihad ya Kiislamu walaani Veto ya Marekani dhidi ya azimio la kusitisha vita Gaza

17:39 - September 19, 2025
Habari ID: 3481253
IQNA – Harakati za mapambano ya ukombozi wa Wapalestina, Hamas na Jihad ya Kiislamu, zimetoa matamko ya kulaani hatua ya Marekani kutumia kura ya turufu au veto kuzuia kupitishwa kwa rasimu ya azimio la kusitisha vita Gaza, wakisema kuwa hatua hiyo inachochea jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika tamko lake, Harakati ya Jihad ya Kiislamu ilisema kuwa matumizi ya kura ya veto na Marekani ili kuzuia kusitishwa kwa mauaji ya kimbari Gaza ni ushahidi mwingine kuwa utawala wa Trump ni mshirika na mfadhili mkuu wa jinai hizi.

“Msimamo wa utawala wa Trump ni wa kupuuza sheria za kimataifa, watu wa eneo hili, na hata serikali za ukanda huu,” tamko hilo liliongeza.

Jihad ya Kiislamu ilieleza kuwa msimamo huo wa Marekani unalingana na juhudi za utawala wa Kizayuni kupanua mashambulizi yake ili kubadilisha sura ya eneo lote.

Hamas nayo ilikemea vikali hatua ya Marekani, ikisema kuwa ni ishara ya ushirikiano wa wazi wa Washington katika jinai ya mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina, na kwamba ni ruhusa ya kuendelea kwa jinai za mauaji, njaa, na mashambulizi ya kikatili dhidi ya Jiji la Gaza.

“Tunashukuru msimamo wa nchi 10 zilizowasilisha rasimu ya azimio hili kwa Baraza la Usalama, na tunaziomba nchi zote pamoja na taasisi za kimataifa kuendelea kushinikiza baraza la jinai la (waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni na serikali yake) Benjamin Netanyahu kusitisha mashambulizi yake, kuzuia kuendelea kwa jinai ya mauaji ya kimbari, na kuhakikisha viongozi wa utawala wa Kizayuni wanawajibishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa kutenda jinai,” Hamas iliongeza.

Katika hatua iliyodhihirisha kutengwa kwa Marekani kimataifa, Alhamisi Marekani ilipiga kura ya veto dhidi ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililodai kusitishwa kwa vita Gaza na kuachiliwa kwa mateka.

Hii ilikuwa mara ya sita kwa Marekani kufanya hivyo kuhusu vita vya Gaza ndani ya chombo hicho chenye nguvu zaidi cha Umoja wa Mataifa.

Wajumbe wote 14 wengine wa Baraza la Usalama walipiga kura ya kuunga mkono rasimu hiyo, ambayo pia ilitaka utawala wa Kizayuni kuondoa vikwazo vyote dhidi ya misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina milioni 2.1 wanaoishi Gaza.

“Upinzani wa Marekani dhidi ya azimio hili si jambo la kushangaza,” alisema Morgan Ortagus, mshauri mkuu wa sera wa Marekani, kabla ya kura kupigwa.

Riyad Mansour, balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, alieleza masikitiko yake kuhusu kura ya veto ya Marekani. “Ninaelewa hasira, huzuni na kukata tamaa kwa watu wa Palestina wanaotazama kikao hiki cha Baraza la Usalama, wakitumaini msaada na mwisho wa jinamizi hili,” alisema Mansour.

Kura hiyo ilifanyika siku chache kabla ya mkutano wa kila mwaka wa viongozi wa dunia katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambapo suala la Gaza litakuwa ajenda kuu, na washirika wakuu wa Marekani wanatarajiwa kutambua rasmi taifa huru la Palestina — hatua ya ishara inayopingwa vikali na Israel na Marekani.

Kura ya veto ya Marekani pia imekuja wakati ambapo takriban nusu ya Wamarekani wanasema kuwa majibu ya kijeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza “yamepitiliza mipaka,” kwa mujibu wa utafiti wa Associated Press-NORC Center for Public Affairs Research.

Rasimu ya azimio hilo, iliyotungwa na nchi 10 wanachama walioteuliwa wa Baraza la Usalama, ilikwenda mbali zaidi ya matoleo ya awali kwa kusisitiza “kuongezeka kwa mateso” ya raia wa Palestina.

Azimio hilo jipya lilieleza “wasiwasi mkubwa” baada ya ripoti ya mwezi uliopita kutoka kwa taasisi kuu ya kimataifa ya masuala ya njaa, ikisema kuwa Jiji la Gaza limekumbwa na baa la njaa, na kwamba njaa hiyo huenda ikaenea kote Gaza bila kusitishwa kwa vita na kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya misaada ya kibinadamu.

Wachambuzi wanaamini kuwa matokeo ya kura ya Alhamisi yanazidi kuonesha kutengwa kwa Marekani na Israel katika jukwaa la kimataifa kuhusu vita vya kimbari vya karibu miaka miwili dhidi ya Gaza.

3494658

 

captcha