IQNA

Katika Kikao Nchi za Kiislamu Doha

Rais wa Iran aonya kuhusu uchokozi wa Israel dhidi ya nchi za Kiislamu

22:46 - September 15, 2025
Habari ID: 3481239
IQNA-Katika kilele cha dharura cha nchi za Kiarabu na Kiislamu kilichofanyika jijini Doha, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, alitoa onyo kali kuhusu mashambulizi ya Israeli ya Septemba 9 dhidi ya Qatar, akisema kuwa tukio hilo linaonyesha wazi kuwa hakuna nchi ya Kiarabu au Kiislamu iliyo salama dhidi ya uchokozi wa utawala wa Tel Aviv.

Akizungumza mbele ya viongozi wa mataifa ya Kiislamu waliokutana leo jijini Doha, Rais Pezeshkian alibaini kuwa mashambulizi hayo yalilenga kuwaua viongozi wa harakati ya Hamas waliokuwa wakijadili pendekezo la Marekani la kusitisha mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Alitaja kitendo hicho kuwa ni “ugaidi wa wazi” na “uchokozi dhidi ya diplomasia,” akisisitiza kuwa Israel inakiuka maadili na sheria za kimataifa bila kujali.

“Shambulio dhidi ya Doha limevuruga hesabu nyingi potofu na kufichua ukweli mchungu: hakuna mji mkuu wa Kiarabu au Kiislamu ulio salama.Uamuzi ni mmoja: lazima tuungane,” alisema Pezeshkian kwa msisitizo.

Rais huyo alieleza kuwa mashambulizi hayo ya kigaidi ni ishara ya kukata tamaa kwa utawala wa Israel, yakitokana na miongo kadhaa ya kinga inayotolewa na baadhi ya mataifa ya Magharibi kupitia msaada wa kidiplomasia, kijeshi na kifedha. Aliongeza kuwa mwaka huu pekee, Israel imefanya mashambulizi katika nchi kadhaa za Kiislamu, kila mara ikijitetea kwa kisingizio cha “kujilinda,” huku mataifa ya Magharibi yakitoa matamshi ya kulaani yasiyo na uzito.

Rais Pezeshkian alifafanua kuwa vitendo vya Israel ni sehemu ya mkakati mpana wa “utawala wa mabavu, maangamizi ya kimbari, na kueneza hofu,” akisema kuwa Marekani na baadhi ya mataifa ya Ulaya ni washirika wa kimkakati katika mpango huo wa upanuzi na uchokozi.

Alitoa wito kwa mataifa ya Kiislamu kuchukua hatua madhubuti: kuisusia Israel, kukata misaada ya kijeshi na kifedha, na kuwashtaki viongozi wake katika mahakama za kimataifa. Hata hivyo, alisisitiza kuwa mafanikio ya hatua hizo yanategemea mshikamano wa kweli.

“Utawala wa Israel umetangaza vita dhidi ya mamlaka yetu, heshima yetu, na mustakabali wetu. Jibu letu ni hili: hatutatishwa, hatutagawanyika, na hatutakaa kimya,” alihitimisha kwa kauli nzito.

Kwa upande wake, Emir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, alilaani mashambulizi hayo akiyataja kuwa ni “ya kisaliti” na “ya kioga,” baada ya vifo vya wanachama watano wa Hamas na afisa mmoja wa usalama wa Qatar.

4305221

captcha