IQNA

Msomi: Kuporomoka kwa elimu na mgawanyiko viliwezesha sera za ukoloni Katika Ulimwengu wa Kiislamu

18:14 - September 15, 2025
Habari ID: 3481236
IQNA – Hujjatul-Islam Ali Abbasi, mjumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu nchini Iran, amesema kuwa madola ya kikoloni ya Magharibi yaliendeleza sera zao katika maeneo ya Waislamu kupitia sababu kuu mbili: kuporomoka kwa elimu miongoni mwa Waislamu na mgawanyiko ndani ya jamii za Kiislamu.

Abbasi, ambaye pia ni rais wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al-Mustafa, alitoa kauli hiyo siku ya Jumapili wakati wa kikao na Imamu wa msikiti mkubwa nchini Burkina Faso. Alisema kuwa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al-Mustafa, kinalenga kuhudumia wanafunzi na wasomi wa elimu za Kiislamu kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Aligusia ukatili wa hivi karibuni wa utawala wa Kizayuni huko Gaza, ambako maelfu wameuawa katika mashambulizi ya Israel. Abbasi alisema, “watu wasio na hatia, wakiwemo wanawake na watoto, wamechinjwa na utawala huu wa uasi pamoja na waungaji mkono wake,” huku mataifa ya Kiislamu na Kiarabu yakibaki kimya kwa kiasi kikubwa.

Alisisitiza kuwa matukio haya si mapya. “Mizizi ya jinai hizi inarudi miaka 75 nyuma, wakati ambapo nchi za Magharibi ziliunda utawala huu wa bandia kupitia makubaliano yao,” alisema.

Abbasi alibainisha kuwa kwa karne nyingi, makabila tofauti na wafuasi wa dini mbalimbali waliishi kwa amani katika eneo hilo, hadi pale serikali za Magharibi zilipoanza kutekeleza sera za ukoloni.

Alitaja Kampuni ya British East India kama mfano, ambayo polepole ilichukua udhibiti wa bara dogo la India. Alieleza kuwa “maendeleo ya kielimu ya Magharibi, sambamba na kudorora kwa elimu miongoni mwa Waislamu na kuibuka kwa migawanyiko ndani ya jamii za Kiislamu, vilikuwa sababu kuu mbili zilizowezesha sera za madola ya kikoloni.”

Sheikh huyo pia alirejea maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisema kuwa Israel bado ni dola linalokalia kwa mabavu maeneo ya Wapalestina. Alitaja uhamishaji wa watu, mauaji, kunyang’anywa ardhi, na kufungwa kwa watu kama ukiukaji wa haki unaoendelea kwa miongo kadhaa. Abbasi aliongeza kuwa mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina bado wanatumaini kurejea katika ardhi zao.

“Bila shaka, iwapo serikali na baadhi ya mataifa zitashirikiana na utawala huu wa bandia, zitakuwa na sehemu ya lawama katika jinai hii ya kihistoria,” alionya.

3494610

Kishikizo: umoja wa kiislamu
captcha