IQNA

Shambulizi la Msikiti Sudan Laua Zaidi ya Raia 70

18:20 - September 20, 2025
Habari ID: 3481255
IQNA – Waasi wa RSF wametekeleza shambulizi la ndege isiyo na rubani dhidi ya msikiti mjini el-Fasher, Sudan, siku ya Ijumaa, na kuwaua zaidi ya raia 70, kwa mujibu wa Baraza la Uongozi la Sudan na waokoaji wa eneo hilo.

Kundi hilo la waasi limeizingira mji huo, ambao ni makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini, tangu siku za mwanzo za mzozo huo.

“Shambulizi la ndege isiyo na rubani lililofanywa na RSF dhidi ya msikiti alfajiri ya Ijumaa mjini el-Fasher limeifanya siku hiyo kuwa miongoni mwa siku za umwagaji damu zaidi tangu kuanza kwa mzingiro wa RSF mwezi Mei mwaka jana,” alisema Hiba Morgan wa Al Jazeera akiripoti kutoka Khartoum, mji mkuu wa Sudan.

“El-Fasher ni ngome ya mwisho ya jeshi katika eneo hilo, na RSF imekuwa ikifanya mashambulizi ya ndege na mizinga, ikilenga maeneo ya kijeshi na kujaribu kuuteka msingi wa kijeshi wa mji huo... Kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya RSF, maeneo ya raia kama hospitali, shule, na vituo vya wakimbizi yameathirika,” aliongeza.

Chumba cha Dharura cha Abu Shouk, mojawapo ya makundi ya kujitolea yanayoratibu misaada nchini Sudan, kilisema kuwa “miili ilitolewa kutoka kwenye kifusi cha msikiti” baada ya shambulizi hilo, huku wakaazi wakiliambia shirika la habari la AFP kuwa walikuwa wakichunguza mabaki ya jengo hilo ili kuwapata na kuwazika waliopoteza maisha.

Kamati za Upinzani za el-Fasher, kundi la raia wa eneo hilo wakiwemo wanaharakati wa haki za binadamu wanaofuatilia ukiukwaji wa haki, walichapisha video mtandaoni ikionyesha sehemu za msikiti zikiwa zimeporomoka na miili kadhaa ikiwa imetapakaa kwenye eneo hilo lililofunikwa na kifusi.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan (Sudan Doctors’ Network) ulilaani shambulizi hilo kama “jinai ya kuchukiza” dhidi ya raia wasio na silaha, likionyesha “kutojali kwa RSF kwa thamani za kibinadamu, kidini na sheria za kimataifa.”

Shambulizi la Ijumaa ni mfululizo wa ghasia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoingia mwaka wake wa tatu kati ya jeshi la Sudan na RSF.

Katika ripoti iliyotolewa Ijumaa, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) ilisema kuwa vifo vya raia na ghasia za kikabila vimeongezeka sana wakati vita vikitimiza miaka miwili katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa raia 3,384 wamefariki katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu, idadi inayokaribia asilimia 80 ya vifo vya raia 4,238 vilivyorekodiwa mwaka mzima wa 2024.

“Mgogoro wa Sudan umesahaulika, na natumai ripoti ya ofisi yangu itaangazia hali hii ya maafa ambapo jinai za kikatili, ikiwemo jinai za kivita, zinaendelea kutekelezwa,” alisema Volker Turk, mkuu wa OHCHR.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa mwenendo wa ghasia za kingono, mashambulizi yasiyo na mwelekeo, na matumizi ya nguvu za kisasi dhidi ya raia, hasa kwa misingi ya kikabila, umeendelea. Pia ilibainisha kuwa matumizi ya ndege zisizo na rubani yameongezeka, hata katika maeneo ya kaskazini na mashariki ya Sudan ambayo awali hayakuwa yameathirika na vita.

“Kuongezeka kwa mgogoro wa kikabila, unaojengwa juu ya ubaguzi na ukosefu wa usawa wa muda mrefu, kunatishia sana uthabiti wa muda mrefu na mshikamano wa kijamii nchini,” alisema Turk.

“Maisha mengi zaidi yataendelea kupotea iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuwalinda raia na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia bila vikwazo.”

Tangu Aprili 2023, vita vya Sudan vimesababisha vifo vya maelfu na kuwafanya takriban watu milioni 12 kuwa wakimbizi. Umoja wa Mataifa umetaja mgogoro huo kuwa miongoni mwa janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani, huku njaa ikizidi katika maeneo ya Darfur na kusini mwa Sudan.

Vita hivyo vimegawanya nchi: jeshi linadhibiti kaskazini, mashariki na katikati, huku RSF ikitawala maeneo ya kusini na karibu yote ya Darfur magharibi.

Juhudi za kusitisha mapigano kati ya pande zinazohasimiana bado hazijazaa matunda. Sudan inatuhumu Umoja wa Falme za Kiarabu  (UAE) kuwa inawaunga mkono waasi wa RSF lakini UAE imekanusha tuhuma hizo.

/3494662

Kishikizo: sudan waasi
captcha