IQNA

Sheikh Zakzaky: Mwamko dhidi ya Unyama wa Israel Gaza umeimarika hata katika nchi za Magharibi

21:41 - September 16, 2025
Habari ID: 3481242
IQNA – Kiongozi wa Harakati za Kiislamu nchini Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky, amesema kumeshuhudiwa ongezeko la mwamko na uungaji mkono kwa Wapalestina katika nchi za Magharibi.

 

“Katika nchi za Magharibi, kwa ujumla watu wameamka na wanapinga jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza. Raia wa mataifa ya Magharibi wamesimama bega kwa bega na wananchi wa Palestina na kulaani unyama unaofanywa dhidi yao,” alisema Sheikh Zakzaky.

Alitaja hatua ya Uhispania kufunga anga yake kwa ndege za Kizayuni kuwa ni ishara njema, na akasisitiza: “Tunatarajia mataifa yote ya Ulaya yatachukua msimamo sawa.”

Akirejelea msaada wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mapambano na wananchi wa Palestina, Sheikh Zakzaky alisema: “Cha kusikitisha ni kwamba hatuoni mshikamano wa dhati kutoka kwa nchi nyingine za Kiislamu kwa ajili ya Wapalestina.”

Aidha alisisitiza umuhimu wa umoja wa Kiislamu dhidi ya utawala wa Kizayuni, akisema: “Wazayuni wanataka kuleta mgawanyiko na mifarakano miongoni mwa Waislamu. Hatua kama Mkutano wa Umoja wa Kiislamu unaofanyika Tehran kila mwaka zinaweza kuvunja vizuizi vya kutoelewana na kuwakutanisha Waislamu kama umma mmoja. Tunatarajia hili litafanikishwa hivi karibuni.”

Sheikh Zakzaky pia alitoa wito kwa nchi za Kiislamu ziweke vikwazo dhidi ya utawala wa Kizayuni na kukata kabisa uhusiano wowote na Tel Aviv.

“Utawala wa Kizayuni ni utawala wa uvamizi. Umevamia ardhi ya Palestina, unajifanya mmiliki wake halali na unaendelea kumwaga damu za wananchi wasio na hatia,” alisisitiza.

Akaongeza: “Ni wajibu sasa kwa nchi za Kiislamu kukata uhusiano wote na utawala huu wa uvamizi; huu ndio wakati wa kuchukua hatua madhubuti.”

Sheikh Zakzaki ameshiriki katika mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Kiislamu ambao umefanyika Tehran hivi karibuni na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya Maulamaa wa Kishia na Ahlul Sunna kutoka kona zote za dunia.

3494615

Habari zinazohusiana
captcha