Taarifa ya pamoja ya Taasisi ya Hija na Ziara ya Iran na Biitha ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kutangaza kuwa, Mahujaji wa Kiirani waliopoteza maisha yao Mina ni 464 zimetoa mkono wa pole kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, taifa la Iran na familia zilizopoteza ndugu zao waliofariki dunia katika maafa ya Mina. Taarifa hiyo imebainisha kuwa, baada ya kupita siku saba tangu kutokea maafa ya Mina na baada ya kufuatilia usiku na mchana katika katika hospitali zote na vituo vya afya katika miji ya Makka, Jeddah, Taif na maeneo ya Mina na Arafat, hali ya Mahujaji wa Kiirani katika tukio hilo imefahamika. Alkhamisi iliyopita kulitokea msongamano mkubwa wa Mahujaji huko Mina wakati walipokuwa wakielekea katika eneo la kupigia mawe shetani na kupelekea maelfu ya Mahujaji kupoteza maisha. Viongozi wa Saudia wanalaumiwa kutokana na uzembe wa usimamizi wa ibada ya Hija ambapo kabla ya hapo kulitokea ajali ya winchi katika msikiti mtakatifu wa Makka na kuua zaidi ya mahujaji 107.