Msafara huo ambao ulianzia Jimbo la Kano wiki iliyopita ulivurugwa na kundi la kitafkiri la Boko Haram ambapo gaidi wa kundi hilo alijirupua na kuua waumini 24. Msafara huo wa Arubaini mwaka huu ulioandaliwa na Harakati ya Kiislamu Nigeria ulitembea masafa ya kilomita 75. Sheikh Ibrahim Usman wa Harakati ya Kiislamu Nigeria amesema msafara huo pia ulijumuisha kiongozi wa Kanisa la Evangelical la Kaduna, Pasta Yohanna Buru.
Wakati huo huo nchini Iraq mamilioni ya wafanyaziara tayari wameshawasili katika mji wa Karbala kwa ajili ya kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein AS. Serikali ya Iraq imeimarisha usalama na imearifiwa kuwa maafisa 35,000 wanalinda doria katika mji huo. Ikumbukwe kuwa takribani miaka 1376 iliyopita, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali (AS) akiwa na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Majlisi za siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walijitolea roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala.