IQNA

Human Rights Watch
12:49 - December 24, 2015
News ID: 3468960
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limekosoa vikali mauaji ya jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu katika mji wa Zaria na kusema hakuna kisingizo chochote kile kinachoweza kutetea ukatili huo.

Taarifa ya shirika hilo imeeleza kuwa, hatua ya jeshi la Nigeria la kuwauwa Waislamu wakiwemo watoto haihalalishiki na kwamba, ni ya kinyama. Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, jeshi la Nigeria liliwashambulia watoto wa Kiislamu kwa risasi bila sababu yoyote.
Katika taarifa iliyotiwa saini na Daniel Bekele, Mkurugenzi wa Human Rights Barani Afrika, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ametakiwa kusitisha ukiukwaji haki za binadamu unaotekelezwa na jeshi la nchi hiyo. "Mauaji ya mamia ya Waislamu wananchama wa Harakati ya Kiislamu Nigeria mikononi mwa jeshi kuanzia Desemba 12 hadi 14 ni jambo lilisolweza kuhalalishika." Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Human Rights Watch imewahoji watu 16 walioshuhudia mauaji hayo ambao wote wamesema jeshi la Nigeria liliwafyatulia risasi Waislamu wa madhehebu ya Shia katika maeneo matatu tafauti mjini Zaria  kaskazini mwa Nigeria."  Human Rights Watch imebaini katika ripoti hiyo kuwa, "Kwa uchache Waislamu 300 waliuawa na kuna uwezekano idadi hiyo ikawa kubwa zaidi. Wanajeshi walizika miili ya waliouawa katika makaburi ya umati pasina idhini ya familia husika na jambo hili linafanya iwe vigumu kubaini idadi hasa ya waliouawa."

Shambulio hilo la kinyama lililopangwa vyema dhidi ya Mashia wa mji wa Zaria limeendelea kuakisiwa kwa wingi ulimwenguni na Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeonya dhidi ya matokeo yake mabaya. Sultan Muhammad Sa'd Abubakr Sokoto, Mkuu wa Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Nigeria ameitahadharisha serikali ya Nigeria dhidi ya kutekeleza hatua ambazo zinaweza kuchochea misimamo mikali nchini humo.

Siku ya Jumanne Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pia ilitoa taarifa ikisema kuwa watu waliojeruhiwa katika tukio hilo la kikatili wangali wanazuiliwa katika vituo vya kijeshi na kuwa wanaendelea kupoteza maisha yao katika vituo hivyo kutokana na majeraha waliyopata na wala hawashughulikiwa kitiba. Ibrahim Musa, msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pia amesema kuwa mali za harakati hiyo katika jimbo la Kaduna zinaendelea kuporwa na kuharibiwa na kuongeza kuwa shule moja pamoja na makaburi ya wanachama wa harakati hiyo yaliharibiwa na jeshi hilo siku ya Jumatatu.

Baada ya kuwashambulia Waislamu katika mji wa Zaria, Jeshi lilifanya shambulizi jingine dhidi ya nyumba ya Sheikh Zakzaki, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Sheikh Zakzaki alipigwa risasi nne na hivi sasa hali yake ni mbaya kiafya huku akiwa mikononi mwa jeshi. Baada ya habari kuenea kuwa Sheikh Zakzaki alikuwa amejeruhiwa vibaya kutokana na hujuma hiyo jeshi lilitagaza kuwa sheikh huyo anapata matibabu katika hospitali moja ya kijeshi.

Lakini katika mazungumzo yake na Idhaa ya Kiarabu ya Radio Tehran, Sheikh Ya'qub Yahya, mwanachama wa Harakat ya Kiislamu amesema kuwa Sheikh Zakzaki bado hajulikani aliko. Amesema uvumi unaoenezwa kwamba huenda sheikh huyo akafunguliwa mashtaka una lengo la kupotosha fikra za waliowengi na kufunika jinai za serikali ya Nigeria. Mwanachama huyo wa Harakati ya Kiislamu amesema kuwa Mawahabi wa Nigeria wameingia katika vita vya pande zote na dhidi ya wafuasi wa Madhehebu ya Ahlul Beit wa Mtume (saw) nchini humo lakini kwamba kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu, dini tukufu ya Kiislamu inaendelea kuongeza na kuimarika kwa kasi kubwa.

3468841

Name:
Email:
* Comment: