IQNA

Katibu Mkuu wa UN ataka matatizo ya wakimbizi Warohingya yatatuliwe kimsingi

19:25 - August 28, 2020
Habari ID: 3473113
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa kutatuliwa tatizo la mgogoro wa wakimbizi Warohingya kupitia utatuzi wa chanzo kikuu cha sababu za wao kukimbia makazi yao nchini Myanmar.

Katika taarifa kupitia msemaji wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anafungamana na wale wote ambao wameathiriwa na magogoro huo huku akisema ataendelea kufanya kazi na wadau wote kuhakikisha kuwa kunapatikana  ustawi endelevu, haki za binadamu na amani nchini Myanmar.

Aidha ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za dharura za kuchunguza chanzo za kuwa wakimbizi jamii ya Waislamu Warohingya huku akisema kunapaswa kuandaliwe mazingira ya kuwawezesha wakimbizi hao wote kurejea makwao kwa amani, kwa hiari, na kwa heshima.

Mapema wiki hii  Waislamu Warohingya ambao ni wakimbizi nchini Bangladesh walishiriki katika 'maandamano ya kimya kimya' kukumbuka mwaka wa tatu tokea waanze kufurushwa makwao nchini Myanmar.

Miaka mitatu iliyopita, yaani Agosti 2017, inadaiwa kuwa wanamgambo walishambulia vituo vya polisi na kituo cha kijeshi katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar ambapo maafisa 12 wa usalama waliuawa.

Jeshi la Myanmar lilitumia kisingizio hicho kuanzisha oparesheni kubwa ya maangamizi ya umati dhidi ya Waislamu Warohingya ambao kwa muda mrefu walikuwa wanakandamizwa na kubaguliwa. Tukio hilo lilipelekea Warohingya 730,000 kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh na kujiunga na wenzao laki mbili ambao katika miaka ya nyuma walikuwa wameikimbia nchi yao.

Umoja wa Mataifa umesema ukandamizaji wa Waislamu nchini Myanmar ambao unatekelezwa na jeshi la nchi hiyo una lengo la maangamizi ya kimbari.

3472398

captcha