IQNA

22:19 - August 22, 2020
Habari ID: 3473092
TEHRAN (IQNA) – Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetoa wito wa kutafutulwia suluhisho jipya na la kudumu kwa wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya walio ndani na nje ya Myanmar.

UNHCR imesema karibu Warohingya 900,000 ni wakimbizi nchini Bangladesh na walifika katika kambi za nchi hiyo kuanzia miaka mitatu iliyopita.

Msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic amesema jamii ya kimataifa ni lazima idumishe uungaji mkono kwa wakimbizi Warohingya na pia kwa jamii ambazo zimewapa kuhifadi sambamba na kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu wakimbizi hao.

Amesema serikali ya Bangladesh imewalinda wakimbizi Warohingya na imewapa misaada ya kibinadamu.

Itakumbukwa kuwa wimbi jipya la mauaji, mashambulizi na ubakaji wa jeshi la Myanmar katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu wa Rohingya, lilianza tarehe 25 Agosti mwaka 2017 ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa. Aidha zaidi ya Waislamu wengine milioni moja wa jamii hiyo walilazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh huku wengine wakipata hifadhi katika nchi kama vile India, Thailand na Malaysia.

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein aliesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Mwezi Januari mwaka huu, Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) imeitaka serikali ya Myanmar kuchukua hatua za dharura za kuzuia mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Rohingya, ikisisitiza kuwa Warohingya hao wamesababishiwa machungu na maumivu yasiyoweza kufutika au kurekebishika.

Akisoma agizo la majaji wote 17 wa mahakama hiyo iliyoko The Hague nchini Uholanzi jana Alkhamisi, Rais wa ICJ, Abdulaqawi Ahmed Yusuf, amesema, "Mynamar imesababisha hasara isiyofidika kwa kukanyaga haki za Warohingya."

Novemba mwaka uliopita, Gambia iliwasilisha faili la kesi ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Warohingya katika mahakama hiyo ya juu ya Umoja wa Mataifa iliyoko The Hague.

3472341/

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: