IQNA

Umoja wa Mataifa walaani ukandamizaji wa Waislamu Warohingya nchini Myanmar

20:59 - September 15, 2020
Habari ID: 3473170
TEHRAN (IQNA) - Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuchukuliwa hatua zaidi kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanyika nchini Myanmar dhidi ya jamii ya Waislamu wa Rohingya.

Michelle Bachelet ambaye alikuwa akizungumza katika kikao cha 45 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva amesema kuwa hujuma na mashambulizi yanayoendelea kufanywa dhidi ya raia katika majimbo ya Rakhine na Chin yanaweza kuorodheshwa katika jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.

Bachelet ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kushughulikia ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa dhidi ya Waislamu waliowachache wa Rohingya nchini Myanmar.

Vilevile amezungumzia kutoweka watu, mauaji ya kiholela ya raia, kufukuzwa watu kwa umati katika makazi yao, kukamatwa kiholela, mateso na mauaji yanayofanyika vizuizini na uharibifu wa mali za raia na kutoa wito wa kukomeshwa uhalifu huo mara moja.

Mashambulizi ya jeshi la Myanmar dhidi ya makazi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika mkoa wa Rokhine hapo 2017 yaliwalazimisha watu zaidi ya laki saba na nusu (750,000) kukimbia makazi yao na kuomba hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Maelfu ya Waislamu hao pia wameuawa katika mashambulizi ya Mabudha wenye misimamo mikali wakishirikiana na vikosi vya jeshi la taifa, na Umoja wa Mataifa unasema maafisa wa kisiasa na kijeshi wa nchi hiyo wanapaswa kufunguliwa mashtaka ya kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu.  

3923024

captcha