IQNA

Kufuatia jinai dhidi ya Waislamu wa Myanmar

Jina Suu Kyi laondolewa katika orodha ya waliopokea tuzo ya Bunge la Ulaya

18:26 - September 11, 2020
Habari ID: 3473157
TEHRAN (IQNA) - Bunge la Umoja wa Ulaya limefuta jina la Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala nchini Myanmar ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo katika orodha ya tuzo ya kifakhari ya taasisi hiyo ya kutunga sheria ya Ulaya.

Bunge la Ulaya limesema limemuondoa Suu Kyi katika orodha ya shakhsia waliotunukiwa tuzo hiyo inayofahamika kama 'Jamii ya Tuzo ya Sakharov' kutokana na hatua yake ya 'kukiri' kuwa serikali imehusika na jinai dhidi ya Waislamu wa jamii wa Rohingya.

Bunge la Umoja wa Ulaya lilimpa Suu Kyi  tuzo hiyo ya juu zaidi ya haki za binadamu mwaka 1990, kutokana na jitihada zake za kupigania demokrasia nchini Myanmar, lakini duru zilizo karibu na Bunge la EU zimesema kuondolewa jina la kiongozi huyo wa Myanmar katika 'Jamii ya Tuzo ya Sakharov' ndivyo vikwazo vya juu zaidi vya taasisi hiyo muhimu ya Ulaya.

Katika hotuba yake ya dakika 30 mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) Disemba mwaka jana, Suu Kyi kwa kiburi alilikingia kifua jeshi la Myanmar, mbali na kukataa kutaja jina la 'Rohingya' kwenye hotuba hiyo iliyokuwa na maneno 3,379, kitendo ambacho wakosoaji wanasema ni muendelezo wa njama za kuwapokonya Waislamu wa Rohingya haki zao na kufuta utambulisho wao.

Disemba mwaka 2018, Jiji la Paris nchini Ufaransa lilichukua uamuzi wa kumnyang'anya uraia wa fahari kiongozi huyo wa chama tawala nchini Myanmar, kutokana na mauaji yanayoendelea kufanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Mwezi mmoja kabla ya hapo, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitangaza kuwa limempokonya Suu Kyi tuzo yake ya juu kabisa ya haki za binadamu ya 'Ambassador of Conscience.'

Aidha wawakilishi wa bunge la Canada huko nyuma walimnyang'anya 'uraia wa fakhari' Suu Kyi, mwezi mmoja baada ya kunyang'anywa tuzo ya Edinburgh, kutokana na hatua yake ya kukataa kulaani jinai kubwa zinazofanywa na jeshi na Mabudha wenye misimamo ya kigaidi wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya.  

Kabla ya hapo Shirika la  Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (ISESCO) lilitaka mwanamke huyo anyang'anywe pia Tuzo ya Amani ya Nobel. Suu Kyi alipewa tuzo ya Nobel mwaka 1991.

Kamati ya Tuzo ya Amani ya Nobel imesema kwa sasa hakuna utaratibu wa kumpokonya tuzo hiyo aliyeipokea.

3922199

captcha