IQNA

Magaidi wahujumu Msikiti Somalia, watu sita wauawa

18:55 - September 11, 2020
Habari ID: 3473159
TEHRAN (IQNA) – Watu wasiopungua sita wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya gaidi kufyatua bomu baada ya swala ya Ijumaa katika msikiti uliooko katika bandari ya Kismayo, kusini mwa Somalia.

Afisa mwandamizi wa polisi Sahal Nur amewaambia waandishi habari kuwa, gaidi aliyekuwa amejifunga mshipi wa mabomu amejilipua karibu na mlango wa msikiti wakati waumini walipokuwa wakiondoka baada ya swala ya Ijumaa leo.

Imedokezwa kuwa gaidi huyo alikuwa alalenga afisa mkuu wa biashara katika eneo hilo, ambayo alijeruhiwa katika hujuma hiyo.

Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hiyo. Kundi la kigaidi la Al Shabab, linalofungamana na Al Qaeda, hutekeleza mashambulizi kama hayo mara kwa mara.

Somalia ilitumbukuia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe karibu miaka 30 iliyopita na magaidi wakufurishaji wa Al Shabab walianzisha hujuma dhidi ya nchi hiyo mwaka 2008.

Askari wa Kulinda Amani wa  Umoja wa Afrika Somalia (AMISOM) wapatao 21,000 wamejitahidi kurejesha utulivu katika nchi hiyo lakini hawajafanikia kuliangamiza kundi la kigaidi la Al Shabab ambalo hutekeleza mashambalizi hatari mara kwa mara nchini humo hasa katika mji mkuu Mogadishu.

3922269/

captcha