IQNA

Watu 8 wauawa katika hujuma ya kigaidi mjini Mogadishu, Somalia

15:35 - November 25, 2021
Habari ID: 3474598
TEHRAN (IQNA) - Kwa uchache watu 8 wameuawa na wengine zaidi ya 15 wamejeruhiwa hii leo katika mlipuko wa bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari karibu na shule moja katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mohamed Abdillahi afisa usalama mjini Mogadishu amethibitisha kujiri hujuma hiyo ya kigaidi na ameongeza kuwa wanafunzi 11 ni miongoni mwa majeruhi. 

Amesema hawafahamu shambulio hilo lilikusudiwa kina nani kwa kuwa kulikuwa na gari ya ulinzi binafsi iliyokuwa ikisindikizwa katika njia hiyo karibu na mahali pa tukio. Wakati huo huo Abdiladir Abdirahman Mkurugenzi wa Huduma za Ambulance za Aamin huko Mogadishu ameutaja mlipuko huo wa bomu kuwa ni maafa. 

Hakuna kundi lililojitokeza na kukiri kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi hata hivyo wanamgambo wa kundi la Al Shabaab wamedai kuhusika na matukio mengine ya milipuko huko Mogadishu likiwemo shambulio kubwa la mauaji la mapema Jumamosi lililosababisha kifo cha mwandishi habari mtajika wa Somalia Abdiaziz Mohamud Guled. Guled alifahamika kama mkosaji mkubwa wa magaidi wa mtandao wa al Qaida.  

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 baada ya kuangushwa utawala wa Siad Barre. Katika miaka ya hivi hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wa al-Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM wanaokadiriwa kufikia 21,000 wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 ili kujaribu kukabiliana na magaidi wa al-Shabab. Hatahivyo pamoja na vitihada hizo za kimataifa, magaidi wa al-Shabab wanaendelea kutekeelza hujuma Somalia na nchi jirani ya Kenya.

4016184/

Kishikizo: somalia ، mogadishu ، magaidi ، al shabab
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha