IQNA

10 Wauawa katika hujuma ya kigaidi ya Al Shabab mjini Mogadishu Somalia

20:27 - July 03, 2021
Habari ID: 3474067
TEHRAN (IQNA)- Watu wasiopungua kumi wameuawa baada kundi la kigaidi la Al Shabab kutekeleza hujuma katika mghahawa mmoja wenye shughuli nyingi kwenye makutano ya barabara ya Jubba, katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Maafisa wa usalama wanasema  gaidi aliyekuwa amejifunga mshipi wa mabomu alijilipua Ijumaa jioni ambapo  mbali na watu kumi kuuawa kwenye mripuko huo uliojiri katika wilaya ya Shibis, wengine wasiopungua tisa wamejeruhiwa.

Kundi la kigaidi la Al Shabab limedai kuhusika na hujuma hiyo ambayo imetekelezwa karibu na makao makuu ya Shirika la Usalama wa Taifa la Somalia.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya watu 12 kuuawa kufuatia mashambulio mawili ya kigaidi yaliyolenga kituo kimoja cha kijeshi na eneo la makazi ya raia katika jimbo la Galmudug, katikati mwa Somalia.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lilitoa taarifa likitangaza kuhusika na mashambulio hayo ambayo limedai yaliua askari 32 wa serikali kuu na ya kieneo. Kundi hilo la kigaidi ambalo liliasisiwa mwaka 2004 lina fikra potovu ambazo zinahusishwa na kundi jingine la kigaidi la al-Qaida.

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 baada ya kuangushwa utawala wa Siad Barre. Katika miaka ya hivi hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wa al-Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM wanaokadiriwa kufikia 21,000 wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 ili kujaribu kukabiliana na magaidi wa al-Shabab. Hatahivyo pamoja na vitihada hizo za kimataifa, magaidi wa al-Shabab wanaendelea kutekeelza hujuma Somalia na nchi jirani ya Kenya.

3475132

captcha