IQNA

Kiongozi Muadhamu atuma salamu za rambirambi baada ya kuaga dunia Ayatullah Misbah Yazdi

11:51 - January 02, 2021
Habari ID: 3473516
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma ujumbe maalumu wa kuomboleza kifo cha mwanachuoni mkubwa, faqihi mwanaharakati, Ayatullah Muhammad Taqi Misbah Yazdi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma ujumbe huo wa tanzia leo Jumamosi na sambamba na kutoa mkono wa pole kufuatia kifo cha mwanachuoni huyo mkubwa kwa familia yake, wanafunzi na wapenzi wake wote, amesema kwamba, Ayatullah Misbah Yazdi alikuwa ni mwanafikra mkubwa, kiongozi mwenye ustahiki, mwenye ufasaha wa lugha na imara katika kutangaza haki na kutotetereka katika njia iliyonyooka.

Ayatullah Khamenei aidha amesema, mchango mkubwa wa Ayatullah Misbah Yazdi kwa kweli alikuwa na sifa za kipekee katika kuzalisha fikra za kidini, kutunga vitabu muhimu sana, kulea wanafunzi bora na kuyapigania Mapinduzi ya Kiislamu kwa nguvu zake zote katika medani zote muhimu na nyeti.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, imani thabiti ya kidini na taqwa ndizo sifa za daima alizokuwa nazo Ayatullah Misbah Yazdi tangu ujanani mwake hadi mwishoni mwa umri wake na alipata taufiki ya kupata mafanikio mazuri katika njia ya maarifa ya tawhidi ikiwa ni atia na zawadi kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa mwanachuoni huyo mwanaharakati.

Ayatullah Muhammad Taqi Misbah Yazdi, mjumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambaye pia alikuwa mkuu wa Taasisi ya Elimu na Utafiti ya Imam Khomeini MA, alifariki dunia jana Ijumaa jioni, Januri 1, 2021, akiwa na umri wa miaka 85.

3944863

captcha