IQNA

Mnasaba

Waislamu wamkumbuka Imam Sadiq (AS) ambaye alitilia mkazo umoja

12:56 - May 16, 2023
Habari ID: 3477005
TEHRAN (IQNA) Waislamu kote duniani hususan wafuasi na wapenzi wa Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad (SAW) leo tarehe 25 Mfunguo Mosi Shawwali wanakumbuka na kuombeleza tukio chungu la kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu, Imam Ja'far Sadiq (AS).

Siku kama ya leo miaka 1296 iliyopita Imam Ja'far Sadiq mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake, aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi Mansur al Dawaniqi. Imam Sadiq alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Muhammad Baqir. Imam Sadiq ambaye kipindi cha uongozi wake kilisadifiana na zama za mapigano makali kati ya watawala wa Kiumawi na Kiabbasi, alitumia fursa hiyo kueneza elimu na maarifa sahihi ya Kiislamu. Alifanikiwa kulea na kutayarisha wasomi hodari katika taaluma mbalimbali kama tiba, kemia, hesabati, nujumu hadithi na kadhalika. Jabiri bin Hayyan ambaye anatambuliwa hii leo kuwa ndiye baba wa elimu ya kemia alikuwa mwanafunzi wa Imam Ja'far Saqid (AS). Ushawishi wa Imam ulienea kwa kasi katika ulimwengu wa Kiislamu, jambo ambalo halikuwafurahisha watawala wa Kiabbasi. Hatimaye mtawala Mansur al Dawaniqi aliamuru Imam apewe sumu. Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa sumu hiyo katika siku kama ya leo na akazikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.

Jukumu la kuongoza umma

Imam Sadiq AS alibeba jukumu la uimamu na kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Muhammad Baqir AS . Kipindi chake kilisadifiana na zama za migogoro na mapigano makali kati ya Bani Umayyah na Bani Abbas ambapo mashinikizo yalipungua kwa Ahlul Bayt wa Mtume SAW. Imam alitumia fursa hiyo kueneza mafundisho sahihi ya Uislamu na kulea wanafunzi hodari katika taaluma mbalimbali kama kemia, hisabati, nujumu na kadhalika. Jabir bin Hayyan ambaye anatambuliwa kuwa baba wa elimu ya kemia pia alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa Imam Jaafar Sadiq (AS).Katika makala hii maalumu tutaangazia machache katika sira ya Imam Sadiq AS kuhusu umoja baina ya Waislamu.Imam Jaafar Sadiq AS alitumia kipindi cha miaka 34 ya umri wake wa miaka 65 kubeba mas-ulia mazito na hasasi ya Uimamu na uongozi wa umma wa Kiislamu. Kati ya Ahlu Bayt wa Bwana Mtume SAW, hakuna yeyote miongoni mwao aliyepata fursa kubwa zaidi kama aliyopata yeye ya kueneza mafundisho ya Uislamu na kuandaa shakhsia wateule na watajika. Zama za Imam Sadiq AS zinaweza kutajwa kuwa ni zama za migongano ya fikra na kuibuka madhehebu na matapo mbalimbali. Jambo hili lingeweza kuikosesha jamii ya Kiislamu mafundisho halisi ya dini hiyo na kuwaelekeza watu kwenye upotofu; lakini kuwepo kwa nuru ya shakhsia ya Imam Jaafar As- Sadiq AS kuling'arisha anga ya fikra za wenye kiu ya haki na kuwaacha vinywa wazi watu waliokuwa wakijigamba kuwa wajuzi wa elimu na maarifa.

Upendo na urafiki

Imam Sadiq AS alikuwa akisistiza kila mara juu ya kuwepo uhusiano wa kiutu na wa upendo mkubwa baina ya watu. Alikuwa akisema: "Shikamaneni, pendaneni, tendeaneni wema na ihsani na oneaneni huruma". Mtukufu huyo alikuwa akiusia mtu kuwa na upendo na urafiki na Waislamu wote; na hata akamuusia mmoja wa masahaba zake kwa kumwambia:" Wafikishie salamu wafuasi wetu na waambie Mwenyezi Mungu anamrehemu mja anayejijengea urafiki kwa watu".Imam Jaafar As-Sadiq AS alikuwa akiamini kwamba watu wa jamii tofauti za kidini ni sehemu ya Jamii ya Kiislamu na wanapaswa kuheshimiwa. Yeye mwenyewe alikuwa katika zama ambazo waliishi ndani yake watu wa dini na madhehebu mbalimbali.

Mwamala na mlahaka

Tunapoutalii mwamala na mlahaka wa Imam Sadiq kwa wafuasi wa dini na madhehebu nyengine tutabaini kwamba mtukufu huyo alikuwa akiwapokea katika darsa zake Waislamu wa madhehebu mbalimbali bali hata na wasiokuwa Waislamu. Abu Hanifa, Imam wa madhehebu ya Hanafi ni miongoni mwa watu hao, ambapo yeye mwenyewe aliwahi kusema, lau isingelikuwa miaka miwili aliyosoma kwenye darsa ya Imam Sadiq AS, basi angeangamia.Mlahaka huo wa Imam Jaafar As-Sadiq AS ulileta faida nyingi sana kwa jamii ya Waislamu wa zama hizo.

Miongoni mwa hizo ilikuwa ni ya watu kukutanika pamoja na kujdiliana, ambapo hata kama majadiliano yao hayakuishia kwa mmoja kukubali fikra na rai ya mwenzake, lakini yalijenga upendo na kuwafanya wamoja. Kwa sababu wakati watu wanapokaliana mbali hufikiriana dhana mbaya, na hilo ni jambo linalochangia sana kuwepo suutafahamu baina yao. Kuonana uso kwa uso kuna taathira kubwa ya kumfanya mtu awe na ufahamu sahihi na wa pande zote wa itikadi na mitazamo ya wenzake.Kuhudhuria darsa za Imam Sadiq AS kuliwafanya watu wenye fikra nyenginezo wamfahamu vizuri na kwa karibu zaidi Imam na kutambua adhama yake ya kielimu na utukufu wake wa kiroho. Kwa hakika sira hiyo ya tadbiri na hekima ya Imam Jaafar As-Sadiq AS inapasa kuwa dira na mwongozo wa kufuatwa na madhehebu mbalimbali; kwani sababu kubwa inayozifanya madhehebu leo hii ziwe mbalimbali ni suutafahamu juu ya itikadi na matendo baina ya madhehebu moja na nyengine.

Umoja wa Waislamu

Na ni suutafahamu hiyo, ndiyo inayotumiwa na maadui kusababisha na kuchochea chuki na uadui baina ya Waislamu wenyewe.Japokuwa watu waliokuwa wakishiriki kwenye darsa za Imam Jaafar As-Sadiq AS hawakuwa na mtazamo sawa kifikra na mtukufu huyo lakini walikuwa wakiitukuza daraja yake ya elimu na kukiri kwamba hawakuwahi kuona faqihi mkubwa zaidi ya Imam. Tab'an kuna idadi kubwa ya wanafunzi na wahudhuriaji wa darsa za Imam Jaafar As-Sadiq waliofuata njia yake. Mfano mmoja maarufu wa wanafunzi hao ni Hisham Ibn Hakam. Vitabu vya hadithi na historia vya Shia na Suni vimesimulia mengi kuhusu midahalo na mijadala aliyofanya Imam Jaafar As-Sadiq AS na viongozi wa madhehebu, wa kidini na hata wasio wa kidini wa zama zake. Lakini nukta muhimu ni kwamba mijadala hiyo haikuishia kwenye utengano wala uhasama.

Kujadiliana na watu kwa upole na kwa wema

Kwani moja ya usuli ya kiakhlaqi ya Imam ilikuwa ni kushikamana na wasia wa Qur'ani usemao "jaadilhum billatii hiya ahsan", yaani kujadiliana na watu kwa upole na kwa wema. Kwa hivyo hata wapinzani wenyewe walikuwa wanakiri kwamba Imam Jaafar Sadiq alikuwa akichunga heshima ya mtu anayejadiliana naye na kusikiliza maneno yake hadi mwisho kwa hamu, utulivu na umakini.Kisha kwa kutumia maneno sahihi na yaliyokamilika, lakini machache na yenye kufikisha ujumbe, ndipo na yeye akawa anabainisha rai na maoni yake.Kuhusu ulazima wa kudumisha umoja na kuwa kitu kimoja, Imam Sadiq AS alimueleza mmoja wa masahaba zake alitwaye Zaid Ibn Hisham kuhusu jinsi ya kulahikiana na kuamiliana na wafuasi wa madhehebu nyengine za Kiislamu kwa kusema:"Ingieni na salini misikitini mwao; watembeleeni wagonjwa wao; shirikini kwenye maziko yao; na kuweni na tabia ya namna itakayowafanya wakujieni na kusali nyuma yenu....Mwenendo wenu utakapokuwa huo watasema, hawa wana madhehebu ya Jaafarii; Mwenyezi Mungu amrehemu Imam Sadiq, amelea wafuasi wazuri walioje.... Lakini kama akhlaqi zenu zitakuwa mbaya;... watasema hawa ni wafuasi wa Jaafari, na Imam Sadiq amelea wafuasi wabaya walioje."Katika mahala pengine Imam Jaafar Sadiq AS amesema: "Muislamu ni ndugu wa Muislamu, na ni sawa na jicho, kioo na muongozo kwake; katu hamsaliti; hamhadai; hamdhulumu; hamwambii uongo na wala hamsengenyi."Kwa hivyo kwa mtazamo wa Imam Jaafar Sadiq AS misingi ya kuimarisha na kuiunganisha jamii ya Waislamu ni kuwa na nia njema, kutakiana kheri, kushirikiana na kusaidiana.

captcha