IQNA

Maarifa ya Manabii

Wajue Manabii wa Mwenyezi Mungu: Idris

17:47 - July 25, 2024
Habari ID: 3479184
IQNA – Kwa mujibu wa riwaya, Nabii Idris (Mwenyezi Mungu Amrehemu-AS-) aliishi kati ya zama za Adam (AS) na Nuh (AS) na alisifika kwa umahiri wake wa sayansi na elimu.

Idris (AS) alikuwa nabii aliyeishi kati ya zama za Adam (AS) na Nuhu (AS). Kulingana na masimulizi, alizaliwa miaka 830 baada ya Adam katika mji wa Misri.

Jina lake limetajwa mara mbili ndani ya Quran: mara moja katika aya “Na mtaje katika Kitabu Idris. Hakika yeye alikuwa mkweli na Nabii,” (Surah Maryam, aya ya 56) na tena katika Aya “Na [kumbukeni] Ismail, Idris, na Dhul-Kifl—kila mmoja wao alikuwa miongoni mwa wanaosubiri.” (Surah Al-Anbiya, aya ya 85)

Jina “Idris” linatokana na neno la Kiarabu “dars,” linalomaanisha “maarifa tele.” Aliitwa Idris kutokana na ujuzi wake mkubwa, kujitolea katika kujifunza, na uvumilivu katika elimu. Inasemekana pia kwamba alisoma sana sheria na desturi za Mwenyezi Mungu.

Idris (AS) alijulikana kwa mchango wake katika uandishi, ualimu, na sayansi. Alikuwa mtu wa kwanza kushona nguo, kwani watu waliomtangulia walitumia ngozi za wanyama kwa nguo.

Pia alifundisha watu jinsi ya kujenga majengo, na alijenga miji kwa msaada wa wanafunzi wake.

Enzi za Idris (AS) hazikuwa na maarifa na utamaduni, na alipewa jukumu na Mwenyezi Mungu kuanzisha sayansi na mbinu za kielimu. Kulingana na masimulizi, alikuwa wa kwanza kuzungumzia mwendo wa nyota na anga na anatajwa kuwa ndiye mwanzilishi wa dawa. Pia alikuwa wa kwanza kuandika kwa kalamu na kutoa hekima na kufundisha elimu ya nyota.

Urithi wa Idris (AS) kama ishara ya sayansi na uvumbuzi unazingatiwa vyema, na anaonekana kuwa mmoja wa viongozi wa mwanzo katika sayansi na mawazo alipokuwa akianzisha sayansi mbalimbali na ujuzi sahihi, wa kimantiki.

Baada ya kuwaita watu kwenye imani ya Mwenyezi Mungu mmoja,  Idris, kama manabii wengine, alitafuta kurekebisha jamii na kushughulikia matatizo ya watu. Alishiriki kikamilifu katika jamii, akitoa msaada na mwongozo. Kwa mfano, alipokuwa Misri, aliwataka watu wamtii Mwenyezi Mungu na kuepuka uovu.

Akiwa na ujuzi wa lugha nyingi, alizitumia kuwasiliana na watu katika lugha zao, akiwafundisha siasa na kuanzisha adabu zinazofaa kwa kila taifa.

3489218

Kishikizo: idris
captcha