
Mkutano huo, ulioandaliwa mjini Kuala Lumpur na Jukwaa la Kimataifa la Umoja na Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu (WFPIST) lenye makao yake Tehran kwa ushirikiano na Baraza la Mashauriano la Mashirika ya Kiislamu Malaysia (MAPIM) pamoja na taasisi zinazounga mkono Palestina, ulihudhuriwa na wanazuoni na wanafikra kutoka nchi za ukanda wa ASEAN.
Akihutubia mkutano huo, Waziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Malaysia, Muhammad bin Sabu, alisisitiza kuwa umoja ni mradi wa kistaarabu na wa kitaasisi, si hisia tu, na kwamba haupaswi kubaki kama kauli mbiu katika hotuba.

Alirejelea pia matukio ya Gaza kama “uharibifu usio na kifani, mauaji ya halaiki na kuporomoka kwa maadili,” akieleza ukubwa wa janga la kibinadamu kama “kinyume chenye uchungu,” huku akitaja maandamano ya kila wiki katika miji mikuu kama London, Paris na New York kuwa ishara kwamba dhamiri ya dunia bado hai.
Habari inayohusiana:
Afisa huyo wa Malaysia alionya kuwa shutuma pekee hazibadilishi hali halisi, na akayataka mataifa ya Kiislamu kurejesha nafasi yao ya kimaadili na ya uongozi katika kutetea haki kwa kuufanya umoja kuwa taasisi halisi na kushikilia misimamo thabiti na ya kimsingi kuhusu Palestina.
Katibu Mkuu wa WFPIST, Hujjatul Islam Hamid Shahriari, alikuwa mzungumzaji aliyefuata. Alisema kuwa Palestina ndiyo dira ya ukweli duniani na inapaswa kutambuliwa kama kipaumbele cha msingi cha kimaadili na kibinadamu.

Alisisitiza kuwa suala la Palestina si la Wapalestina pekee, bali ni suala la ubinadamu wote. Aliongeza kuwa, “Suala la Palestina ni mtihani wa kimaadili, kibinadamu na kistaarabu kwa ulimwengu wa Kiislamu na jamii ya kimataifa. Sio suala la kisiasa tu, bali ni mapambano ya msingi kati ya haki na dhuluma. Palestina ni dira ya ukweli duniani na lazima itambuliwe kama kipaumbele cha kimaadili na kibinadamu.” Mwanazuoni huyo pia alisema kuwa umoja wa Kiislamu unajengwa juu ya maadili ya pamoja, misimamo ya wastani, mazungumzo na ushirikiano kati ya madhehebu za Kiislamu, na hivyo hakuna ulazima wa kuwa na mtazamo unaofanana.
Habari inayohusiana:
“Umoja hauhitaji kuondoa tofauti, bali kugeuza utofauti kuwa nguvu kupitia mazungumzo ya kimantiki na maridhiano,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa MAPIM, Sheikh Azmi Abdul Hamid, katika hotuba yake alisisitiza haja ya kuubadilisha umoja kutoka kauli mbiu hadi mkakati wa kivitendo.
Alisema kuwa umoja unahitaji “mwelekeo wa pamoja, nidhamu na uwajibikaji,” na akaongeza kuwa umoja wa leo lazima ujumuishwe katika simulizi la pamoja, shinikizo la kisiasa, hatua za kiuchumi, mipango ya kisheria na majibu ya kibinadamu.

Alibaini kuwa suala la Palestina si la kisiasa pekee, alisisitiza kwamba mradi Msikiti wa Al-Aqsa bado uko chini ya uvamizi na Gaza iko chini ya mzingiro, Ummah hauwezi kudai uongozi wa kimaadili.
Alilalamika kuwa janga la Palestina limeendelea kwa zaidi ya miaka 75, si kwa sababu ya nguvu ya uvamizi pekee, bali pia kutokana na mgawanyiko, uzembe na wakati mwingine ukimya wa Ummah wa Kiislamu.
Aidha, alielezea hali ya Gaza kama “ishara ya kuporomoka kwa utaratibu wa maadili ya kimataifa” na akakosoa kile alichokiita “sheria za kimataifa zinazotumika kwa kuchagua.”
4329608