Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo wakati alipotembelea maonyesho ya mafanikio ya kikosi cha anga na anga za mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kusema mbele ya makamanda wa jeshi hilo kuwa, katika mazungumzo yanayoendelea kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1, Wamagharibi wamezuka na tamaa mpya za kutaka Iran iwekee kikomo mipango yake ya makombora licha ya kwamba madola hayo siku zote yanatoa vitisho vya kijeshi dhidi ya Iran, ndio maana kuwa na matarajio hayo ni upumbuvu wa mwisho.
Amesema, vipaji, uwezo na nia ya kweli ni mambo muhimu kwa ajili ya kuimarisha nguvu za kila taifa na amewataka viongozi wote wa Iran, kadiri watakavyokuwa na ubunifu na kufanya jitihada mbalimbali katika siasa za nje na mabadilishano ya kimataifa, lakini watambue kuwa hawapaswi kuyakwamisha na mazungumzo mahitaji ya Iran na baadhi ya masuala kama vikwazo, bali watafute njia nyingine za kutatua masuala hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, uadui dhidi ya taifa la Iran unatokana na kuwa taifa hili limeamua kuwa huru na kushikamana na Uislamu na Qur'ani.
Ameongeza kuwa: Uislamu na Qur'ani inayataka mataifa ya Waislamu kusimama imara juu ya miguu yao wenyewe na wategemee utambulisho wao wa Kiislamu, kibinadamu na kuwa na imani na Mwenyezi Mungu na kutokubali kudhindwa na dhulma ya kimataifa, hivyo maadamu taifa la Iran litaendelea kushikamana na Uislamu, Qur'ani na malengo yake matukufu, basi uadui wa mabeberu nao utaendelea kuwepo.