Hussein Ja’ffar al-Hulu mshindi wa tano katika mashindano ya usomaji Qur’ani ya Tehran yaliyofanyika miaka mitano iliyopita amesema, kufanyika kwa mashindano hayo kuna umuhimu mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Amesema mashindano hayo yanawashirikisha hata washindani kutoka Saudi Arabia ambayo ina Mawahabi wenye misimamo ya kupindukia mipaka na ya kiuadui moja kwa moja dhidi ya Mashia. Amesema mashindano hayo yanayofanyika kwa uungaji mkono mkubwa wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuwashirikisha wanachuo wa Kiislamu kutoka pembe mbalimbali za dunia yana athari kubwa katika kuleta umoja miongoni mwa Waislamu. Amesema kuhudhuria wasomaji mashuhuri wa Qur’ani katika mashindano hayo na mchango wao katika usomaji wa kitabu hicho cha mbinguni katika mashindano hayo kumetoa mvuto maalumu kwa wanachuo wa Kiislamu wanaoshindana katika mashindano hayo. Al-Hulu ambaye pia ni mshindi wa kwanza wa mashindano ya kitaifa ya usomaji Qur’ani nchini Iraq, anaamini kwamba, Shahat Muhammad ndiye msomaji bora zaidi wa Qur’ani katika ulimwengu wa Kiislamu kutokana na lahani na tuni yake ya kuvutia anaposoma kitabu hicho kitakatifu. Amesema sauti ya msomaji wa Qur’ani ina athari kubwa kwa msikilizaji na kwamba hata huenda ikawafanya watu wasiozingatia Qur’ani kuanza kutafuta njia za kujifunza mafundisho ya kitabu hicho. Amesema kuna umuhimu wa kujifunza maana ya maneno na aya za Qur’ani kwa sababu bila ya kufanya hivyo si rahisi kwa wasikilizaji na wasomaji na hata kwa Waarabu wenyewe kufahamu maana halisi ya kitabu hicho. 318540