IQNA

Washindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Ushairi ya ‘Imamu Shahidi’ Watunukiwa

22:35 - July 15, 2026
Habari ID: 3482491
IQNA – Washindi wa duru ya kwanza ya Tuzo ya Kimataifa ya Ushairi ya “Imamu Shahidi” walitangazwa na kutunukiwa katika hafla iliyofanyika mjini Tehran siku ya Jumanne.

Tuzo hiyo, iliyoandaliwa na Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu (ICRO), inajumuisha mashairi ya washairi kutoka nchi mbalimbali waliotunga mashairi kuhusu Kiongozi shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Akihutubia hafla hiyo, mkuu wa ICRO Hujjat al-Islam Mohammad Mehdi Imanipour amesema kuwa tuzo hiyo ilikuwa tukio la kwanza kufanyika baada ya maziko ya Kiongozi huyo shahidi, na kwa mujibu wa matarajio, kuna uwezekano wa kuandaa hafla kama hiyo pia katika nchi nyingine.

Amesisitiza kuwa haja ya kueleza namna Imamu shahidi alivyoutilia umuhimu ushairi si kubwa, kwani alikuwa akiamini kuwa ujumbe hufikishwa vyema zaidi kupitia ushairi.

Hujjat al-Islam Imanipour ameongeza kuwa Kiongozi shahidi alikuwa akiutazama ulimi wa Kifarsi na fasihi yake kuwa ni nuru ya mamlaka ya ustaarabu wa Kiirani na Kiislamu, jambo ambalo ni mtazamo wa kipekee.

Amesema: “Takriban miaka miwili iliyopita nilifanya safari kwenda Moscow kwa ajili ya mazungumzo ya baina ya dini, ambapo nilikutana na Askofu Mkuu wa Russia, ambaye alisema kwamba mnapaswa kuwasilisha fikra za kiongozi wenu kwa njia mbalimbali na kuzieneza katika nyanja tofauti.”

Amesisitiza kuwa hapaswi kuwepo upungufu wa maarifa kuhusu Imamu huyo shahidi.

Akirejelea idadi ya mashairi yaliyowasilishwa katika tuzo hiyo, Hujjat al-Islam Imanipour amesema kuwa katika mkutano na waandishi wa habari siku chache zilizopita idadi ya mashairi ilikuwa 2,000, na leo imefikia mashairi 3,000, jambo linaloashiria mapokezi mapana ya tukio hilo.

Gholam Ali Haddad Adel, mkuu wa Taasisi ya Saadi, alikuwa miongoni mwa waliohutubia hafla hiyo.

Amesema kuwa Kiongozi shahidi alikuwa akiamini kwamba mshairi hawezi kuwa asiyejali maumivu na mateso ya watu, wala kushuhudia dhulma kisha akanyamaza; bali anapaswa kutumia nguvu ya athari ya sanaa yake katika kukabiliana na maadui na madhalimu.

Haddad Adel ameongeza kuwa Kiongozi shahidi alikuwa akiuchukulia ushairi kuwa ni jambo la msingi kwa maadili ya kibinadamu.

Ameendelea kusema kuwa kuandika mashairi kuhusu Kiongozi shahidi ni kuandika kuhusu alama iliyo wazi ya maadili ya kibinadamu.

Wakati huo huo, Alireza Qazveh, katibu wa tuzo hiyo ya kimataifa ya ushairi, katika hotuba yake amewashukuru washairi, taasisi za kitamaduni na wote walioshiriki katika maandalizi ya hafla hiyo, na kusifu mapokezi makubwa kutoka kwa washairi wa Iran na wa kigeni.

Amesema idadi ya kazi zilizopokelewa ni kubwa sana, na bado ipo nafasi ya kukamilisha na kupanua diwani ya mashairi ya washairi wa Iran na wa dunia.

Akirejelea uchapishaji wa mkusanyiko wa kwanza wa kazi za tukio hilo, Qazveh amesema kuwa katika hatua ya kwanza, mkusanyiko wa juzuu 10 umeandaliwa kwa ushirikiano na makundi mbalimbali ya fasihi.

Ameongeza: Sehemu mbalimbali za mkusanyiko huo, zikiwemo mashairi ya Kifarsi, Kiingereza, Kiarabu, mashairi ya Afghanistan, mashairi ya bara Hindi, pamoja na mashairi ya watoto na vijana, zimekusanywa kwa ushiriki wa kundi la washairi, watafiti na wataalamu wa fasihi.

Sayyid Abbas Salehi, Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Iran, pia alihutubia hafla hiyo, akimtaja Kiongozi shahidi kuwa ni “baba wa watu huru wa dunia, Umma wa Kiislamu, na taifa la Iran.”

Ameongeza kuwa jamii ya kifasihi na washairi, kuliko wengine wengi, wanaomboleza kuondokewa na shakhsia iliyojitolea maisha yake kuunga mkono ushairi, fasihi na utamaduni wa Kiislamu na Kiirani.

Salehi ametoa shukrani zake kwa waandaaji, wageni wa ndani na wa nje, na wote walioshiriki katika kuandaa hafla hiyo ya kitamaduni, na kusema: “Kiongozi mwenye hikima wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa miongoni mwa viongozi wachache wa zama hizi duniani waliokuwa na uhusiano wa kina na mapenzi makubwa kwa ushairi na fasihi.”

3498268

Habari zinazohusiana
captcha