Akizungumza katika kikao cha pamoja cha ujumbe wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq, kilichofanyika Alhamisi jijini Tehran wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Iraq Ali al-Zaidi, Pezeshkian amesema ukarimu mkubwa wa wananchi na serikali ya Iraq kwa mamilioni ya mazuwaru wa Kiirani wakati wa matembezi ya kila mwaka ya Arbaeen umeumba mandhari zisizo na mfano za huruma, udugu na mshikamano, ambazo zinastaajabisha ulimwengu na zinastahili kuthaminiwa.
Pia alirejelea ushiriki mkubwa na wa kuvutia wa wananchi wa Iraq katika hafla ya mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, akieleza kuwa ushiriki huo ni alama ya undani wa mahusiano ya kihistoria, kiutamaduni na kidini kati ya mataifa hayo mawili.
Amesema mandhari kama hayo yanaakisi mafungamano ya mizizi ya kina ambayo, mbali na uhusiano wa kisiasa, yameendelea kuyaunganisha mataifa ya Iran na Iraq.
Rais alieleza kufurahishwa kwake kwa kumpokea mwenyeji Waziri Mkuu wa Iraq pamoja na ujumbe aliofuatana nao katika kikao hicho cha pamoja, na akasisitiza azma ya nchi hizo mbili ya kuimarisha kikamilifu uhusiano wao.
Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka uhusiano kati ya Tehran na Baghdad uinuliwe hadi kiwango cha juu kabisa kinachowezekana katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kibiashara, kisayansi, kilimo, viwanda, usalama na miundombinu, kwa kutegemea msingi wa kihistoria, kiutamaduni na kidini wa mataifa hayo mawili.
Akisisitiza ulazima wa kuhuisha zaidi mifumo ya pamoja kati ya nchi hizo mbili, rais ametoa wito wa kuundwa mara kwa mara kwa tume za pamoja na kuharakishwa kwa utekelezaji wa makubaliano ya pande mbili na hati za maelewano. Amesema ni lazima makubaliano yote yaingie katika hatua ya utekelezaji haraka iwezekanavyo kupitia ufuatiliaji endelevu wa taasisi husika, na kwamba mawaziri wanaohusika wanapaswa kuharakisha mchakato wa kukuza ushirikiano kwa kutoa suluhisho za kivitendo.
Rais Pezeshkian pia amesisitiza umuhimu wa kuandaliwa kwa “mpango kamili wa kimkakati wa ushirikiano” kati ya Iran na Iraq, na akauona kuwa ni ramani-elekezi ya kuendeleza mahusiano ya muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
Rais ameutaja usalama kuwa ni miongoni mwa nyanja muhimu zaidi za ushirikiano kati ya Tehran na Baghdad, huku akisisitiza kuwa usalama wa nchi hizo mbili umefungamana.
“Ukosefu wa usalama katika mojawapo ya nchi hizi mbili utakuwa na athari za moja kwa moja kwa nyingine; kwa hivyo, kuendeleza ushirikiano wa kiusalama ni dharura ya kimkakati kwa pande zote mbili.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Iraq amesisitiza nafasi maalumu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika sera ya mambo ya nje ya nchi yake, na kueleza kuwa kuendelezwa na kuimarishwa kwa ushirikiano wa pande mbili ni ulazima wa kimkakati.
Al-Zaidi amesisitiza kuwa usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran una umuhimu wa pekee kwa Iraq, na akasema hakuna sehemu yoyote katika ardhi ya Iraq itakayeruhusiwa kuwa kitovu cha vitisho au cha kusababisha ukosefu wa usalama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Waziri Mkuu huyo wa Iraq pia amerejelea nafasi ya Iran katika mapambano dhidi ya ugaidi, na kusema taifa la Iraq halitasahau kamwe uungaji mkono wa Iran katika kukabiliana na kundi la kigaidi la Daesh (ISIL/ISIS); uungaji mkono ambao haukuishia katika misimamo ya kisiasa pekee, bali ulitolewa kwa vitendo sambamba na wananchi wa Iraq kwa ajili ya kung’oa ugaidi.
Arbaeen ni maadhimisho matukufu ya kidini yanayofanywa na Waislamu, hususan wa madhehebu ya Shia, katika siku ya arubaini baada ya Siku ya Ashura, kuadhimisha kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imam wa tatu wa Waislamu wa madhehebu a Shia.
Hii ni moja ya ziyara kubwa zaidi za kila mwaka ulimwenguni, ambapo mamilioni ya Waislamu wa Shia, pamoja na idadi kubwa ya Masunni na wafuasi wa dini nyinginezo, hutembea kwa miguu kuelekea mji mtukufu wa Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen inasadifia tarehe 4 Agosti.
3498388