IQNA

Zaidi ya Mawakib 13,500 zasajiliwa kutoa huduma katika Matembezi ya Arbaeen

15:49 - July 25, 2026
Habari ID: 3482534
IQNA – Zaidi ya Mawakib (vituo vya kutoa huduma bila malipo) 13,500 kutoka mikoa mbalimbali ya Iraq, pamoja na kutoka mataifa ya Kiarabu, Kiislamu na nchi nyingine za kigeni, zimesajiliwa kushiriki katika maonyesho na matembezi ya Arbaeen ya mwaka huu.

Mawkib (kwa wingi Mawakib) kimsingi ni mahema au vituo vinavyowekwa kando ya barabara zinazoelekea mji mtukufu wa Karbala na ndani ya mji huo wenyewe, kwa ajili ya kutoa huduma za chakula cha nadhiri, vinywaji, malazi, na huduma nyinginezo bila malipo kwa mazuwari wa Arbaeen.

Idara ya Mawakib na Vikundi vya Maombolezo ya Imam Hussein (AS), iliyo chini ya Idara ya Mfawidhi au Usimamizi Mtukufu (Astan) wa Haram Takatifu ya Imam Hussein (AS), imetangaza kusajiliwa kwa zaidi ya Mawakib 13,500 kutoka ndani na nje ya Iraq hadi sasa.

Mohammad Karim Aziz, mkuu wa idara hiyo, alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa baadhi ya Mawakib ambazo bado hazijasajiliwa, idadi hiyo inatarajiwa kupita 16,000.

Aziz alieleza kuwa idara hiyo imetangaza ratiba ya kuwasili kwa vikundi vya maombolezo na Mawakib kwa mujibu wa mfumo maalum uliowekwa na Kamati Kuu, inayojumuisha Wasimamizi wa Haram za Imam Hussein (AS) na Hadhrat Abbas (AS) pamoja na vyombo vya serikali vinavyohusika.

Alibainisha kuwa ratiba ya kuwasili kwa vikundi vya maombolezo imepangwa kulingana na mikoa na nchi mbalimbali ili harakati za mazuwari na maandamano katika uwanja mtakatifu wa Haram ya Imam Hussein (AS) na eneo lililo kati ya Haram mbili takatifu (Bain-ul-Haramain) ziweze kufanyika kwa utaratibu mzuri na kwa wepesi.

Alisisitiza kuwa Usimamizi Mtukufu (Astan) wa Haram ya Imam Hussein (AS) umewataka wasimamizi wote wa Mawakeb na vikundi vya maombolezo kuzingatia maelekezo yaliyotolewa, ikiwa ni pamoja na sifa za magari, ukubwa na nguvu ya vipaza sauti, njia za kuingilia, kuhakikisha vikundi vinaingia kupitia mageti maalum yaliyotengwa, na kufikia viwango vya juu kabisa vya nidhamu na usahihi.

Afisa huyo alisema lengo la kutekeleza kanuni hizi ni kuonyesha sura halisi na adhimu ya ibada na mila za maombolezo ya Ki-Husseini mbele ya walimwengu, na kudhihirisha kiwango cha juu cha nidhamu, uratibu, na uzingatiaji wa sheria katika kuendesha ibada ya Arbaeen.

Katika mfumo wa juhudi hizi za kupanga mambo, Usimamizi Mtukufu wa Haram ya Imam Hussein (AS) unaendelea na juhudi zake za kuweka mazingira bora zaidi kwa ajili ya kupokea vikundi vya maombolezo, kuhakikisha mtiririko mzuri wa harakati, kulinda utakatifu wa ibada hizi, na kuakisi picha ya kistaarabu ya ziara ya Arbaeen kwa ulimwengu, alieleza.

Arbaeen ni tukio la kidini linaloadhimishwa na Waislamu wa Kishia katika siku ya arobaini baada ya Siku ya Ashura, kukumbuka kuuawa shahidi kwa Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imam wa tatu wa Waislamu wa Kishia.

Hii ni moja ya ziara kubwa zaidi za kidini za kila mwaka ulimwenguni ambapo mamilioni ya Waislamu wa Kishia, pamoja na Waislamu wengi wa Sunni na wafuasi wa dini nyinginezo, hutembea kwa miguu kwenda Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arbaeen itakuwa tarehe 4 Agosti.

3498393

captcha