IQNA

Vatikani yapinga madai ya Balozi wa Trump kuhusu Ukosoaji wa Papa kwa Vita dhidi ya Iran

17:05 - July 14, 2026
Habari ID: 3482484
Pope Leo XIV
IQNA – Vatikani (Vatican) imekataa jaribio la balozi wa utawala wa Trump katika Vatikan la kuwasilisha ukosoaji wa Papa Leo wa XIV dhidi ya vita vya Marekani dhidi ya Iran kana kwamba ulikuwa uingiliaji wa kisiasa badala ya msimamo wa kidini.

Jibu hilo lilikuja kupitia makala ya maoni iliyoandikwa na Andrea Tornielli, msimamizi wa uhariri wa Dikasteri ya Mawasiliano ya Vatikani.

Makala ya Tornielli ilifuatia matamshi ya Balozi wa Marekani Vatikani, Brian Burch, aliyedai kuwa Papa Leo alizungumza kimsingi katika nafasi yake ya mtawala wa Jiji la Vatikani.

Burch, ambaye ni mwanaharakati Mkatoliki wa kisiasa na mshirika wa Rais wa Marekani Donald Trump, alisema hivyo basi ukosoaji wa Papa unapaswa kueleweka kwa namna ileile kama maoni yatolewayo na kiongozi mwingine yeyote wa kisiasa.

“Papa anapotenda kama kiongozi mtawala wa Kiti Kitakatifu, anakuwa sawa kwa hadhi na viongozi wa ulimwengu,” Burch alisema katika mahojiano yaliyochapishwa Alhamisi na gazeti la The New York Times.

Tornielli alipinga moja kwa moja tafsiri hiyo katika makala iliyochapishwa na Vatican News, chombo rasmi cha habari cha 'Kiti Kitakatifu'.

Ijapokuwa hakumtaja Burch kwa jina, Tornielli alisema kuwa kumchora Papa kimsingi kama mkuu wa dola kunapotosha asili ya mamlaka yake na kudhoofisha maana ya kiroho ya kauli zake za hadhara.

“Utukuzi wowote au kupindukia katika kuikuza nafasi ya Papa kama mkuu wa dola, na msisitizo wowote juu ya umuhimu wa nafasi hiyo, ni … jambo la kupotosha, kwa sababu hufanyika kwa gharama ya dhamira yake ya kweli pekee kama Mchungaji wa wote,” Tornielli aliandika.

Aliongeza kuwa kauli za Papa kuhusu migogoro ya kimataifa, uhamiaji, na mabadiliko ya kiteknolojia zapaswa kutazamwa kama sehemu ya ujumbe wake wa kidini, wala si diplomasia ya kawaida.

“Hata anapozungumzia vita na amani, uhamiaji au namna ya kubaki na ubinadamu katika zama za akili mnemba, Mrithi wa Petro hubakia, kabla ya yote, kuwa kiongozi wa kiroho,” Tornielli aliandika.

Mjadala huu unaakisi mvutano unaozidi kujitokeza kati ya Papa Leo, Papa wa kwanza mzaliwa wa Marekani, na utawala wa Trump.

Papa Leo amerudia mara kadhaa kukosoa vita vya Marekani dhidi ya Iran, na pia amelaani juhudi za Washington za kulitumia dini kuhalalisha kampeni hiyo ya kijeshi.

3498244

Habari zinazohusiana
captcha