IQNA

Makala 500 za utafiti zawasilishwa katika Kongamano la 6 la Kimataifa la Afya katika Arbaeen

23:31 - July 15, 2026
Habari ID: 3482493
TEHRAN – Mkuu wa kamati ya kisayansi ya Kongamano la 6 la Kimataifa la “Afya katika Arubaini” ametangaza kuwa jumla ya karatasi za utafiti 500 zimewasilishwa katika sekretarieti ya kongamano hilo.

Bi. Vahideh Moradi amesema kuwa katika toleo hili la kongamano, kutakuwa na vikao 12 vya majadiliano (panels) na warsha saba maalum.

Amebainisha kuwa miongoni mwa mada zitakazojadiliwa katika toleo hili ni mafunzo kwa maafisa wa Moukeb (vituo vya huduma kwa mahujaji) na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (AI) katika safari ya Arbaeen

Bi. Moradi amesema kongamano hilo litafanyika siku ya Jumapili na Jumatatu, Julai 19 na 20, katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Iran.

Akielezea mageuzi ya kongamano hili, alisema: “Katika miaka ya awali ya uanzishwaji wa kongamano hili, kwa vile tulikuwa kwenye hatua za mwanzo za kuandaa mada za afya kwa ajili ya Arubaini, tulilenga zaidi masuala ya msingi ya kiafya. Lengo letu lilikuwa kuhakikisha kuwa timu za wataalamu zinazotoa huduma za afya wakati wa matembezi ya Arbaeen zinaweza kunufaika na makala za utafiti na maarifa yaliyozalishwa katika fani hii.”

Aliongeza: “Hata hivyo, mafunzo tuliyopata na uzoefu ambao tumekuwa tukikusanya kila mwaka wakati wa Arbaeen, yamesababisha maboresho makubwa katika uelewa wa umma na huduma za wahudumu wa afya. Kwa msingi huo, mbinu tofauti huandaliwa kwa ajili ya kongamano kila mwaka, na mwaka huu, mada bunifu zitajadiliwa kwa mara ya kwanza katika kongamano hili.”

Arbaeen ni tukio adhimu la kidini linaloadhimishwa aghalabu na Waislamu wa madhehebu ya Shia siku ya arubaini baada ya Siku ya Ashura, ambayo ni kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) na Imamu wa tatu katika madhehebu ya Shia.

Hii ni miongoni mwa mijumuiko mikubwa zaidi za kila mwaka duniani, ambapo mamilioni ya Waislamu wa Kishia, sambamba na Waislamu wengi wa Kisunni na wafuasi wa dini nyingine, husafiri kwa miguu kuelekea Karbala kutoka miji mbalimbali ya Iraq na nchi jirani. Mwaka huu, siku ya Arubaini itaangukia tarehe 4 Agosti.

3498261

captcha