IQNA

Mwanaharakati wa Kenya: Kiongozi Shahidi alikuwa shujaa wa waliodhulumiwa

16:08 - July 25, 2026
Habari ID: 3482536
IQNA – Booker Ngesa Omole, mwanaharakati wa kisiasa kutoka Kenya, amesifu fikra na turathi za Kiongozi aliyeuawa shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, akimtaja Shahidi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuwa shujaa wa waliodhulumiwa.

Omole alisema kuwa fikra za Shahidi Ayatullah Khamenei za kupinga ubeberu pamoja na msimamo wake wa muqawama zitaendelea kuwa na athari katika duru za kielimu na kisiasa.

Akirejelea mitazamo ya kiongozi huyo shahidi kuhusu demokrasia ya kidini na demokrasia huria ya Magharibi, Omole alisema kuwa demokrasia haipaswi kufasiriwa kwa mujibu wa fikra za madola yenye nguvu pekee, akiongeza kwamba mataifa dhaifu nayo pia yana mawazo yenye thamani, na hata bora zaidi katika baadhi ya nyanja.

Alisisitiza kuwa Shahidi Ayatullah Khamenei hapaswi kuangaliwa tu kama kiongozi wa Iran au wa ulimwengu wa Kiislamu, bali pia kama mwakilishi na shujaa wa watu waliodhulumiwa, hususan wa mataifa ya Kusini mwa Ulimwengu.

Omole pia ameangazia uungaji mkono wa dhati wa Kiongozi Shahidi kwa kadhia ya Palestina, akimtaja kuwa miongoni mwa sauti zilizo thabiti zaidi katika kutetea haki za Wapalestina.

Omole amesema kuwa kusoma na kutafakari fikra za Shahidi Khamenei kulimsaidia kuelewa kwa undani zaidi uhalisia wa utawala ghasibu Kizayuni na suala la Palestina.

Ameongeza kuwa si lazima mtu awe Muislamu ili asimame kwa mshikamano na watu wa Palestina.

Aidha, amesema kuwa fikra za Shahidi Imam Khamenei zilisaidia kupanua uungaji mkono kwa Palestina nje ya mipaka ya dini, na zikahimiza umoja miongoni mwa wote wanaounga mkono kwa dhati kadhia ya Palestina.

Omole amehitimisha kwa kusema kuwa Kiongozi Shahidi alisisitiza daima kwamba mapambano ya Palestina hayawezi kutenganishwa na mapambano mapana ya watu waliodhulumiwa ulimwenguni, bali ni sehemu isiyotenganika ya kadhia hiyo hiyo.

Chanzo: Khamenei.ir

captcha