IQNA

Mashambulizi dhidi ya Msikiti mmoja kila baada ya siku tano Uingereza

15:27 - July 25, 2026
Habari ID: 3482532
IQNA – Taasisi ya British Muslim Trust (BMT) imebainisha kuwa, kwa wastani, msikiti mmoja hushambuliwa kila baada ya siku tano nchini Uingereza.

BMT, ambayo ni mshirika rasmi wa serikali ya Uingereza katika kufuatilia vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu (Islamophobia), imerekodi zaidi ya matukio 70 katika kipindi cha miezi 12 iliyopita. Matukio hayo yanajumuisha mashambulizi ya kimwili, uharibifu wa mali, na uchomaji moto makusudi, huku maeneo ya London, Greater Manchester, na West Midlands yakiongoza kwa idadi ya mashambulizi hayo dhidi ya nyumba za Allah.

Miongoni mwa matukio yaliyoripotiwa ni pamoja na lile la mwanaume mmoja aliyeteketeza moto msikiti mmoja huko Peacehaven, Sussex Mashariki, mnamo mwezi Oktoba 2025. Aidha, mnamo Julai 2025, mwanaume mwingine aliwaachia panya nje ya msikiti mmoja huko Sheffield kama kitendo cha kukebehi na kuvunjia heshima taasisi za Kiislamu.

Mwezi Februari mwaka huu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza (Home Office) iliahidi kutoa kiasi cha pauni milioni 40 kwa ajili ya kuimarisha ulinzi, ikiwemo kuajiri walinzi, kufunga kamera za usalama (CCTV), ving’ora, na hatua nyinginezo katika misikiti, shule za Kiislamu, na vituo vya kijamii kupitia mpango wa “Mpango wa Ulinzi na Usalama wa Misikiti” (Protective Security for Mosques Scheme).

Hata hivyo, taasisi ya BMT imelalamika kuwa misikiti inatakiwa kutoa ushahidi kuwa imevamiwa au kulengwa kabla ya kuruhusiwa kupata fedha hizo za ulinzi. Misikiti mingine imesubiri kwa hadi miezi 18 bila kupata msaada huo, huku mingine ikinyimwa kabisa bila maelezo yoyote ya kimsingi kutoka kwa mamlaka husika.

Akizungumzia takwimu hizi mpya, Akeela Ahmed, Mtendaji Mkuu wa BMT, alisema: “Tunaamini kuwa serikali inapaswa kufanya kila liwezekanalo kusaidia misikiti kujilinda… Ni lazima tutambue kuwa kasi ya mashambulizi haya inaongezeka, na tunapaswa kuchukua hatua madhubuti na kujiandaa kukabiliana nayo.”

Aliongeza kuwa: “Msikiti unakuwa hatarini kwa sababu tu ni msikiti… Tunapendekeza kutafuta njia bora zaidi za kufikisha ufadhili huu kwenye misikiti, ikiwemo ugatuaji wa mfuko huu ili kuharakisha utoaji wa huduma.”

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ameliambia gazeti la The Guardian: “Tunafanya kazi ya kushughulikia maombi yote kwa haraka iwezekanavyo.”

3498397

captcha