Katika mahojiano ya kipekee na IQNA, Sergei Zagrobelny, ambaye alikuwa mjini Tehran kuhudhuria shughuli za kumuaga Kiongozi huyo shahidi, alisisitiza nafasi tukufu ya Shahidi Khamenei katika kuimarisha mshikamano na kuishi kwa amani miongoni mwa wafuasi wa dini mbalimbali.
Zagrobelny, ambaye pia ni mwakilishi wa Kyrgyzstan katika Kundi la Haki za Binadamu la Asia ya Kati, alifafanua mtazamo wa Kiongozi shahidi kuhusu ushirikiano wa kidini kwa kusema: “Sisi katika Uislamu na Ukristo tunaye Mwenyezi Mungu mmoja, na kila mwenye maarifa ya Vitabu Vitakatifu anafahamu kuwa ndani yake kumewekwa wazi mwongozo wa jinsi binadamu wanavyopaswa kuhusiana. Kwa hakika, watu wenye imani ya dini wanapaswa kuwa na mtazamo wa umoja na heshima kwa wenzao. Sisi hatuangalii mtu anaamini nini kwa undani, kwa sababu misingi ya imani iliyobainishwa katika Vitabu Vitakatifu iko wazi na haina shaka.”
Alisisitiza kuwa Kiongozi shahidi alikuwa akihimiza daima adabu na heshima kwa matukufu ya dini. “Tunatambua kuwa alikuwa na mtazamo wa kuheshimu dini mbalimbali na viongozi wake; na ndiyo sababu kuu iliyowafanya wawakilishi wa madhehebu na dini tofauti kujitokeza Tehran kutoa heshima zao za mwisho.”
Katika tathmini yake kuhusu uwepo wa wajumbe wa kimataifa katika hafla hiyo ya kumuaga Kiongozi shahidi, Zagrobelny aliitaja Iran kama chimbuko la ustaarabu na kiroho. Alibainisha kuwa Iran ni taifa lenye urithi mkubwa wa kiroho, sambamba na urithi adhimu wa kihistoria na fasihi, kama vile Shahnameh ya Ferdowsi.
“Katika Shahnameh ya Ferdowsi, tunaona wazi kuwa viongozi na watawala wa serikali lazima waongoze kwa kuzingatia malengo ya Kiungu. Pale mwelekeo huu unapokuwepo katika utawala wa nchi, basi taifa zima huwa nyuma ya serikali yao. Hakika, ni mwelekeo huu ndio ulioruhusu Iran kushika nafasi ya kwanza miongoni mwa staarabu za dunia, na tunashuhudia mwendelezo wa misingi hiyo nchini Iran hadi leo hii.”
Katika sehemu nyingine ya mahojiano, kiongozi huyo wa Kikristo aligusia uhuru wanaofurahia raia wa Kikristo nchini Iran na juhudi za Kiongozi shahidi katika kuhakikisha haki zao zinalindwa kwa dhati.
Zagrobelny alihitimisha kwa kugusia mgongano uliopo kati ya madola makubwa ya kibeberu na thamani za kimaadili na kidini, akisema: “Kuna baadhi ya madola ya ulimwengu ambayo lengo lao kuu ni kuharibu mataifa; na ili kufanikisha hili, wanaanza kwa kushambulia thamani za kibinadamu na misingi mikuu ya serikali. Ndiyo maana tunaona kuwa madola haya ya kibeberu, ambayo yanapinga thamani za kibinadamu, taasisi ya familia, na dini, yote yameungana na yanachukua hatua za uhasama dhidi ya nchi kama Iran na Urusi.”
3498203