IQNA

Waislamu nchini Australia waitaka serikali kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu

17:16 - July 19, 2026
Habari ID: 3482509
australia
IQNA – Watetezi wa haki za Waislamu nchini Australia wametoa wito wa kutengwa kwa bajeti mpya na ya kutosha kwa ajili ya programu za kupambana na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia), kufuatia hatua ya Chama cha Labour kukubali sehemu tu ya mpango uliopendekezwa na balozi maalum wa kushughulikia tatizo hilo.

Shirikisho la Mabaraza ya Kiislamu ya Australia limesema kuwa ahadi ya serikali ya shirikisho ya kuchukua hatua juu ya mapendekezo 35 kati ya 54 yaliyoainishwa katika ripoti ya Balozi Maalum, Aftab Malik, ni hatua inayotambua kuwa chuki dhidi ya Waislamu ni tatizo kubwa la kitaifa linalohitaji kushughulikiwa.

Hata hivyo, kundi hilo, ambalo ni chombo kikuu cha Waislamu nchini humo, limesema mwitikio wa serikali haukutosheleza katika nyanja muhimu na limetoa wito wa maelezo zaidi kuhusu jinsi viongozi wanavyopanga kushughulikia mapendekezo yote yaliyotolewa na Balozi Maalum huyo.

Shirikisho hilo limebainisha kuwa mwitikio wa serikali umeishia katika idadi ndogo ya ahadi mpya, zikiambatana na upanuzi wa programu ambazo tayari zilikuwepo na kazi ambazo tayari zinafanywa na ofisi ya balozi huyo, jambo ambalo halitoshi kukabiliana na mizizi ya chuki hiyo.

Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Kiislamu ya Australia, Rateb Jneid, alikuwa ametoa wito wa kufanyika kwa tathmini huru ya sheria za kupambana na ugaidi, pamoja na kuundwa kwa tume ya uchunguzi kuhusu chuki dhidi ya Uislamu, na ubaguzi wa rangi dhidi ya Wapalestina na Waarabu. Wito huo hata hivyo haukupatiwa majibu yoyote miezi 10 tangu ripoti hiyo ilipowasilishwa kwa serikali.

Katika kile kinachoonekana kama hatua ya awali, serikali imejitolea kupitia upya mtaala wa shule za Australia ili kubaini fursa za kuimarisha uelewa na kuondoa aina zote za chuki katika jamii.

3498328

Habari zinazohusiana
captcha