IQNA

Matembezi ya waliofanikiwa kuhifadi Qur'ani Tukufu Nchini Morocco

15:16 - July 22, 2026
Habari ID: 3482525
IQNA– Katika mwendelezo wa kuenzi utamaduni wa kuhifadhi Qur'ani Tukufu, matembezi makubwa ya wahifadhi wa Qur'ani yamefanyika katika mji wa Tifelt, Morocco, ili kusherehekea wahitimu waliofanikiwa kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu. Tukio hilo la kiroho liliambatana na mahudhurio ya viongozi wa kidini, maafisa wa serikali, na wakazi wa mji huo, kama ilivyoripotiwa na Tifeltpress.

Matembezi  hayo yaliyojaa utukufu yaliandaliwa chini ya kaulimbiu ya Aya ya 9 ya Surah Al-Hijr: “Sisi ndio tulioteremsha Ukumbusho (Quran) na Sisi ndio tutakaouhifadhi.” Sherehe hizi pia ziliambatana na maadhimisho ya karne ya 15 tangu kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).

Shule ya Qur'ani iliyo chini ya Msikiti wa Al-Quds mjini Tifelt ilishirikiana kwa karibu na Baraza la Wanazuoni wa Khamisat, mwakilishi wa Wizara ya Awqaf na Masuala ya Kiislamu ya Morocco, pamoja na maafisa wa usalama na serikali za mitaa, kufanikisha hafla hiyo. Msafara huo ulianzia katika jengo la manispaa ya Tifelt kuelekea Msikiti wa Al-Quds, huku wananchi wakijipanga barabarani kushuhudia tukio hilo la kipekee.

Vikosi vya Usalama vya Kitaifa viliongoza msafara huo, vikihakikisha ulinzi thabiti na utaratibu katika maeneo yote ya njia. Katika hali iliyojaa nuru ya imani, washiriki waliimba kasida na nyimbo za sifa za Mtume Mtukufu Muhammad (SAW), wakijenga mazingira ya kiroho yaliyogusa nyoyo za wengi.

Wahifadhi hao walionekana wakiwa wamevalia mavazi ya asili ya kiheshima, wakiwa wamepanda farasi huku wakiwa wamebeba mbao zao za Qur'ani (Alwhi), tukio lililodhihirisha hadhi ya shule za jadi za Qur'ani nchini Morocco. Ni ishara ya fahari na wito kwa vijana kuendeleza njia hiyo tukufu ya kujifunza na kuhifadhi Qur'ani.

Programu hii ni tukio la kila mwaka ambalo linaimarisha nafasi ya shule za Qur'ani katika jamii ya Morocco, huku likiangazia jukumu lao kuu la kulea vizazi kwa misingi ya Kiislamu, kuhifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na kusambaza maadili ya wastani na uvumilivu.

Familia za wahifadhi na washiriki walionyesha kuridhishwa sana na sherehe hizi, ambazo zinaakisi heshima kubwa ambayo jamii ya Morocco inawapa wale wanaojitolea kwa ajili ya Qur'ani. Walisisitiza kuwa hatua kama hizi zinasaidia kuimarisha utambulisho wa kidini na kitaifa, na kuwahamasisha vizazi vijana kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kufuata mafundisho yake mema.

3498363

Kishikizo: morocoo qurani tukufu
captcha