IQNA

Iran yalipiza kisasi, yashambulia kambi za kijeshi za Marekani katike eneo

9:42 - July 12, 2026
Habari ID: 3482473
IQNA-Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo asubuhi vimetekeleza operesheni ya pamoja ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini Jordan, Kuwait, Qatar, Oman na Bahrain, ikiwa ni hatua ya kujibu mashambulizi endelevu ya Marekani dhidi ya maeneo ya kusini mwa Iran.

Katika taarifa ya pamoja, vikosi vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Jeshi la Iran vimetoa onyo kali kuwa hatua yoyote ya ziada ya Marekani itakabiliwa na jibu kali zaidi.

Katika taarifa iliyotolewa mapema Jumapili, Ofisi ya Uhusiano wa Umma ya IRGC imesema kuwa Marekani imethubutu “kujaribu tena kile ambacho tayari kimekwisha jaribiwa” kwa kuilazimisha serikali ya Oman na kuchochea mvutano kupitia “harakati haramu” ya meli kadhaa kusini mwa Lango la Hormuz.

IRGC imeongeza  kuwa, Jeshi la Majini la Iran limefanikiwa kuzima jaribio hilo kwa “jibu madhubuti.”

Taarifa hiyo imebainisha zaidi kuwa Marekani ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya vituo kadhaa vya mwambao na minara ya mawasiliano kando ya pwani ya kusini ya Iran kama majibu ya kushindwa huko.

Kulingana na IRGC, Kikosi cha Anga cha RGC kimelenga miundombinu muhimu ya kijeshi ya Marekani katika Kambi ya Anga ya Mwanamfalme Hassan nchini Jordan wakati wa awamu ya kwanza ya operesheni hiyo ya kulipiza kisasi.

IRGC imeongeza kuwa wakati wa awamu ya pili ya operesheni yake ya kulipiza kisasi, makombora yake ya balistiki pia yamelenga kambi ya kimkakati ya Marekani ya Al Udeid nchini Qatar, na kuharibu kituo cha matengenezo na ukarabati wa ndege za kivita pamoja na kamandi ya kambi hiyo.

Taarifa hiyo imeonya kuwa: “Adui wa Kimarekani na Kizayuni anapaswa kufahamu kuwa mwendelezo wa uchokozi wake utaleta majibu ya kusambaratisha zaidi. Sisi tuko tayari kwa lolote.”

Katika taarifa tofauti, Ofisi ya Uhusiano wa Umma ya Jeshi la Iran imetangaza kuwa imevurumisha ndege zisizo na rubani za kujitoa muhanga dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Kuwait na Bahrain, ikiwa ni jibu la mashambulizi ya mara kwa mara ya Marekani katika maeneo ya kusini mwa Iran.

Jeshi limesema ndege zake zisizo na rubani zililenga mfumo wa ulinzi wa anga wa Patriot, ghala la silaha, na kituo cha rada cha kijeshi cha Marekani nchini Kuwait.

Aidha, wimbi lingine la ndege zisizo na rubani lililenga mfumo wa mawasiliano ya kijeshi ya Marekani na kituo cha rada nchini Bahrain.

Kwingineko, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) limetangaza kuambaratisha vituo vya usambazaji na ukarabati wa meli za kivita za Marekani nchini Oman

Katika taarifa yake, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kuwa limefanikiwa kusambaratisha vituo vya usambazaji wa vifaa (logistics) na majukwaa ya kuongeza mafuta ya meli za kivita za Marekani katika Bandari ya Duqm nchini Oman, kupitia shambulizi zito na la kushtukiza.

“Azimio lenu dhabiti, ambalo lilidhihirika wazi katika maandamano ya kihistoria ya mamilioni ya watu yaliyoushangaza ulimwengu, sasa limejionyesha kupitia ushujaa wa wapiganaji wenu.”

Katika awamu ya tatu ya jibu la operesheni dhidi ya uchokozi wa jeshi la Marekani—jeshi ambalo limekuwa likiua watoto—wapiganaji wa Jeshi la Anga la IRGC wamevipiga na kuviharibu vibaya vituo vya usambazaji wa vifaa vya meli hizo na majukwaa ya kuongeza mafuta ya meli za kubeba ndege za Marekani katika Bandari ya Duqm, Oman, kupitia shambulizi zito na la kushtukiza.

Operesheni hizi za kulipiza kisasi zimekuja saa chache baada ya jeshi la Marekani kuanza tena vitendo vya uchokozi visivyo na sababu dhidi ya kusini mwa Iran. Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) imesema kuwa imetekeleza mashambulizi hayo kwa amri ya Rais wa Marekani Donald Trump, kwa lengo linalodaiwa la kupunguza uwezo wa Iran wa kudhibiti Lango la Hormuz.

Muda mfupi kabla ya tangazo hilo, wakazi katika miji ya bandari ya Asalouyeh na Bandar Dayyer katika Mkoa wa Bushehr waliripoti kusikia milipuko kadhaa.

3498209

Kishikizo: irgc marekani iran
captcha