IQNA-Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Kupambana na Misimamo Mikali kimeonyesha wasiwasi mkubwa kufuatia ongezeko la matamshi ya chuki na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) wakati wa michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2026.
Katika ripoti yake kuhusu suala hili, kituo hicho kilichoko nchini Misri, kimeonya dhidi ya kuongezeka kwa matamshi ya kibaguzi na ya kikaidi yanayohusiana na matukio makubwa ya michezo. Kimesisitiza kuwa matumizi mabaya ya majukwaa ya kidijitali (cyberspace) kusambaza chuki na uchochezi dhidi ya wengine, yanatishia thamani za kuishi kwa pamoja na wingi wa watu katika jamii, na kubadilisha michezo kutoka chombo cha kuleta ukaribu na kuwa jukwaa la kuchochea migawanyiko.
Kituo hicho kimesema kuwa kupambana na janga hili kunahitaji juhudi za pamoja kati ya serikali, mifumo ya mitandao ya kijamii, na taasisi za kijamii ili kujenga msimamo wa uwajibikaji, kuzuia matumizi mabaya ya matukio ya michezo kwa ajili ya kueneza chuki na ubaguzi wa kijinsia au kidini.
Ripoti hiyo pia imebainisha matokeo ya Kituo cha Uhispania cha Kupambana na Ubaguzi na Chuki dhidi ya Wageni, kilicho chini ya usimamizi wa Wizara ya Usalama wa Jamii na Uhamiaji ya nchi hiyo, kuhusu ongezeko la matamshi ya chuki na chuki dhidi ya Uislamu kwenye mitandao ya kijamii katika kipindi cha kuelekea Kombe la Dunia la 2026.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mnamo mwezi Juni, zaidi ya visa 40,000 vya matamshi ya chuki viligunduliwa mtandaoni, ambapo matukio ya michezo yakichukua nafasi ya pili kwa kusababisha aina hii ya maudhui kwa asilimia 16, ikifuatiwa na masuala yanayohusiana na ukosefu wa usalama, ambayo yaliongoza orodha hiyo kwa asilimia 69.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa watu wenye asili ya Afrika Kaskazini walikuwa kundi lililolengwa zaidi, kwa asilimia 88 ya maudhui yote yaliyofuatiliwa, ikifuatiwa na jumbe dhidi ya Waislamu kwa asilimia 11, na kisha maudhui ya kashfa dhidi ya watu wenye asili ya Afrika kwa asilimia 7.
Aidha, ripoti hiyo ilionyesha ongezeko la ukali wa matamshi ya kibaguzi, ambapo asilimia 48 ya jumbe zilizotumika zilikuwa na lugha ya kushusha utu na matusi ya moja kwa moja, huku asilimia 32 ya machapisho yakionyesha makundi yaliyolengwa kama tishio kwa jamii, na asilimia 10 yakitoa wito wa wazi wa kufukuzwa kwa wageni.
Kuhusu mwitikio wa mifumo ya mitandao ya kijamii, ripoti hiyo ilionyesha kuwa asilimia 61 ya maudhui yaliyoripotiwa yaliondolewa. TikTok ilirekodi kiwango cha juu zaidi cha mwitikio kwa asilimia 98, ikifuatiwa na X kwa asilimia 93, Facebook kwa asilimia 62, na Instagram kwa asilimia 32. YouTube ilikuwa na kiwango cha chini kabisa cha mwitikio kwa asilimia 8 pekee.
Kituo hicho kilisisitiza kuwa kupambana na matamshi ya chuki katika ulimwengu wa kidijitali kunahitaji kuendeleza mifumo ya ufuatiliaji na utoaji taarifa, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, na kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa kuheshimu utofauti wa kitamaduni na kidini. Hii kwa upande wake, itahifadhi roho ya ushindani wa kiungwana (sportsmanship) na thamani za kuishi kwa pamoja kati ya watu.
3498381