Shirika la Habari la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limeripoti kutoka mjini Beirut kwamba, Allama Fadhlullah amekosoa vikali kuhudhuria makatili na watenda jinai kama Shimon Peres katika kikao hicho na kuongeza kuwa, kikao hicho kinapasa kuwajumuisha wanazuoni wa kidini tu bila ya kuwashirikisha wanasiasa kama hao walio na rekodi mbovu ya mauaji. Kikao hicho kinatazamiwa kuanza leo tarehe 12 Novemba kwa usimamizi wa Saudi Arabia. Fadlullah amesema kuwa kuketi kando ya watenda jinai kama hao katika kikao cha New York, waovu ambao wametekeleza mauaji ya kutisha dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina na Lebanon na wangali pia wanaendeleza jinai zao dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza kwa kuwazingira kutoka kila upande, ni ishara kuwa washiriki wa kikao hicho wanaunga mkono, kwa njia isiyo ya moja kwa moja, jinai za waovu hao dhidi ya watu wasio na hatia. Amesisitiza kwamba, kufanyika vikao kama hivyo au vya kiuchumi na kuwashirikisha watenda jinai kama hao ni njia moja ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
Huku akielezea mshangao na masikitiko yake makubwa kuhusiana na jambo hilo, mapema Salim al-Hoss, Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon pia alibainisha upinzani wake mkali dhidi ya hatua ya Saudi Arabia ya kumualika Shimon Peres na Tzipi Livni, Rais na Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala wa Israel, kwa utaratibu, katika kikao hicho na kusema kuwa jambo hilo linaenda kinyume kabisa na msimamo wa ulimwengu wa Kiarabu. Katika kikao kingine kama hicho kilichoandaliwa na Saudia nchini Hispania, ni viongozi wa kidini tu, wakiwemo makuhani wa Israel, ndio walioalikwa kushiriki, lakini nchi hiyo ya kifalme mara hii imechukua hatua isiyotarajiwa na ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu kwa kuwaalika wanasiasa, wakiwemo makatili wa Israel, kushiriki katika kikao cha New York.